1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan na waasi wasaini makubaliano ya amani ya Darfur

Halima Nyanza15 Julai 2011

Siku moja tu baada ya Serikali ya Sudan na waasi wa nchi hiyo wa kundi la Liberation and Justice Movement kusaini makubaliano ya amani juu ya jimbo la magharibi la nchi hiyo la Darfur. pongezi zimeanza kutolewa.

https://p.dw.com/p/11vvu
Mazungumzo ya amaniPicha: picture alliance/dpa

Marekani imeyapongeza makubaliano hayo ya amani kati ya serikali ya Sudan na waasi wa Darfur na kuyataka makundi mengine ya waasi yanayokosoa makubaliano hayo, kuingia katika majadiliano.

Makubaliano hayo yalisainiwa jana jioni katika mji mkuu wa Qatar, Doha ambayo nchi hiyo ndiyo iliyokuwa msuluhishi wa mazungumzo ya kutafuta amani ambapo mfalme wa nchi hiyo Hamad bin Khalifa na Rais wa Sudan Omar al-Bashir walikuwepo pia kushuhudia.

Darfur-Rebellen auf Patrouille im Süden Darfurs
Wapiganaji wa DarfurPicha: picture alliance/dpa

Akizungumza baada ya utiaji saini humo, mfalme wa Qatar alisema wakati umefika sasa wa watu wa Darfur kufutahia amani na kuweza kurudi katika nyumba zao walizozikimbia kutokana na mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe.

Tukio hilo pia lilihudhuriwa pia na viongozi wengine wa Afrika kutoka nchi za Chad, Ethiopia, Burkina Faso, Eritrea pamoja na wawakilishi wa mashirika yaliyo katika kanda hiyo.

Mazungumzo hayo pia yalifadhiliwa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Jumuia ya kiarabu.

Katika taarifa yake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani Mark Toner amesema makubaliano hayo ni hatua nzuri kuelekea katika upatikanaji wa ufumbuzi wa kudumu katika mzozo huo wa Darfur.

Aidha amesema wataendelea kuyashinikiza makundi yote ya wapiganaji ambayo yalikataa kushiriki katika mazungumzo hayo ya amani, hususan kundi la waasi la Sudan Liberation Army linaloongozwa na Abdelwahid Nur and Minni Minnawi, kuweza kushiriki kikamilifu katika mpango huo wa amani.

Ameitaka Sudan pia kuonesha udhati wake wa majadiliano zaidi kuweza kupatikana kwa amani Darfur.

Kwa upande wake Abdelwahid Nur amesema wanayapinga makubaliano hayo na kwamba yatavunjika wakati wowote, kutokana na kwamba hayawawakilishi watu wa Darfur.

Kundi nyingine la waasi ambalo pia halikuwa katika mazungumzo hayo ya amani ni lile la Justice and Equality Movement, -JEM- ambalo lilisema kuwa masuala yaliyosainiwa katika mkataba huo hayakidhi matakwa yote ya wa Darfur.

Lakini hata hivyo mmmoja wa wawakilishi wa kundi la waasi ambalo jana lilisaini makubaliano hayola Liberation and Justice Movement alisema wanaamini nyaraka hizo zilizosainiwa zinaelezea masuala yote yanayowahusu watu wa Darfur. Amesema maendeleo ndio kilikuwa chanzo cha mzozo wa Darfur, na kwamba suala hilo limejadiliwa kwa kina na uwazi.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa watu zaidi ya laki tatu wameuawa katika mapigano hayo, huku Sudan yenyewe ikisema ni watu elfu 10 tu. Huku wengine mamilioni wakikimbia makaazi yao.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,afp, Reuters)

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman