1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan ya Kusini yafikia makubaliano na waasi

Admin.WagnerD6 Januari 2011

Sudan ya Kusini imekubaliana waasi wanaotaka kuitenga kusitisha mapigano na kupunguza wasiwasi wa uwezekano wa kuzuka ghasia siku chache kabla ya Kura Maoni ya Jumapili (9 Januari 2011).

https://p.dw.com/p/zuIS

George Athor, afisa mwandamizi wa zamani katika jeshi la kusini mwa Sudan, amekuwa kiongozi wa mwisho wa kundi la wapiganaji wa chini kwa chini ambaye amekuwa akipigana dhidi ya uongozi wa kusini mwa Sudan. Athor, ambaye anaaminika kuwa amejificha katika maeneo ya msituni ya jimbo la Jonglei, alituma ujumbe ambao ulitia saini makubaliano hayo jana Jumatano katika hoteli moja katika mji mkuu wa eneo la kusini wa Juba.

Wapiganaji wa jeshi la Serikali ya Sudan ya Kusini
Wapiganaji wa jeshi la Serikali ya Sudan ya KusiniPicha: AP

Majeshi yake yamewauwa wanajeshi kadha wa jeshi la kusini mwa Sudan tangu pale alipojitenga na serikali ya eneo hilo, baada ya kuwashutumu maafisa kwa kufanya udanganyifu katika uchaguzi wa mwezi Aprili.

Upigaji kura ya maoni utaanza Januari 9, ambapo wapigaji kura wanaulizwa iwapo eneo la kusini liwe huru ama la, ikiwa ni kilele cha hatua za kuleta amani ambazo zilianza mwaka 2005 na kumaliza vita virefu kabisa vya wenyewe kwa wenyewe katika bara la Afrika.

Eneo hilo lenye mafuta , lakini ambalo ni masikini la kusini limekuwa halina usalama kutokana na ghasia za kikabila, wanajeshi wasio na nidhamu pamoja na wapiganaji wengine wanaoipinga serikali na kusababisha hali ya wasi wasi kwamba eneo hilo litapata taabu kujitawala.

Kiasi cha wapigakura milioni 3.9 ambao wamejiandikisha , watapiga kura kuanzia Jumapili ijayo, na kuhitimisha miezi kadha ya matayarisho kwa ajili ya kura hiyo ambayo umoja wa mataifa umesema jana kuwa unatarajia utafanyika bila ya matukio mabaya.

Wasudan ya kusini wengine 60,000 wanaoishi nje ya nchi hiyo wamejiandikisha kupiga kura katika nchi nane duniani, ikiwa ni pamoja na Canada, Ethiopia, Marekani , Australia na Uingereza. Waziri wa utamaduni wa kusini mwa Sudan, Gabriel Chang, alikuwa mmoja wa maafisa wa kusini mwa Sudan jana katika maandamano ya kuwataka watu wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Upigaji kura unatarajiwa kuendelea hadi Januari 15.

Marekani inaamini kuwa kura hiyo ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan ya Kusini itafanyika bila matatizo na kwa njia ya amani, amesema afisa mmoja mwandamizi wa Marekani jana.

Kugawanyika kwa nchi hiyo kunatarajiwa na wengi lakini upande wa kaskazini umeahidi kukubali matokeo ya kura hiyo na kupunguza wasi wasi wa kuzuka tena mzozo mpya.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa zaidi ya waangalizi wa kigeni 1,000 na 15,000 kutoka ndani ya Sudan wataangalia kura hiyo katika vituo 2,700 vya kupigia kura katika Sudan ya kusini pamoja na vituo 175 katika eneo la Sudan ya Kaskazini. Matokeo yatapatikana baadaye mwezi wa Februari.

Mwandishi: Sekione Kitojo/AFPE/DPAE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo