1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yapinga kushirikiana na mahakama ya kimataifa kuhusu wahalifu wa Darfur

Mwakideu, Alex4 Juni 2008

Huku baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likiendelea na ziara yake katika nchi zenye mizozo barani Afrika imebainika kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kuiwekea vikwazo Sudan

https://p.dw.com/p/EDZy
Jimbo la Darfur linalokabiliwa na mizozoPicha: AP

Mabishano yameibuka kati ya nchi hiyo na mahakama ya kimataifa kuhusu mchango wa serikali katika mzozo wa Darfur.


Mjumbe wa sudan katika Umoja wa Mataifa Abdalmahmood Mohamed  amemshutumu mwendesha mashtaka mkuu katika mahakama ya kimataifa Luis Moreno-Ocampo akisema anaharibu mpango wa amani kwa kuzua mashtaka ya uongo.


Mohamed alikuwa anajibu matamko ya Ocampo kwamba serikali nzima ya Sudan imechangia uhalifu dhidi ya binaadamu katika jimbo la Darfur.


Mabishano hayo yanakuja wakati baraza la usalama la umoja wa mataifa linatembelea maeneo ya kaskazini na kusini mwa nchi hiyo kukagua mpango wa amani.


Mjumbe wa ufaransa katika Umoja wa Mataifa Jean-Maurice Ripert, ameishutumu hatua ya Sudan ya kukataa kuwafikisha washukiwa wa uhalifu wa Darfur mbele ya mahakama ya kimataifa akitishia kwamba nchi yake na Umoja wa Ulaya huenda zikaipatia adhabu kali sudan iwapo haitashirikiana.


Miaka mitatu iliyopita baraza la usalama la umoja wa Mataifa lilipendekeza kesi za Darfur zisikizwe katika mahakama ya kimataifa. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametumia ziara ya baraza hilo mjini Khartoum kushinikiza kutekelezwa kwa pendekezo hilo.


Sudan imekuwa ikipinga kusikizwa kwa kesi za Darfur katika mahakama ya kimataifa na imesema imetenga mahakama yake ambayo itazisikiza.


Baadhi ya viongozi wa serikali ambao wanatakikana kufika mbele ya mahakama ya kimataifa ni Haroun na Kosheib ambao wamefunguliwa mashtaka 51 yakiwemo kuua, kubaka, na kuwatesa watu.


Wajumbe 15 wanaojumlisha baraza la usalama la umoja wa mataifa leo wamekutana na waziri wa nchi za nje Deng Alor na makamu wa rais Ali Osman.


Mwaka uliopita Marekani ilitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuungana nayo na kuiwekea vikwazo vya kifedha Sudan.


Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu 300, 000 wameuwawa na wengine milioni 2.2 wamachwa bila makao tangu mzozo wa Darfur ulipoanza mnamo februari mwaka wa 2003.


Balozi wa Kenya nchini Somalia Bethwell Kiplagat ambaye pia ni mpatanishi anaetambulika ulimwenguni anasema ushirikiano wa Umoja wa Afrika na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa unaweza kuleta mabadiliko.


Mapema wiki hii baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilianza ziara yake ya siku 10 katika nchi zinazokabiliwa na mizozo Afrika.


Somalia ni moja wapo wa nchi zilizojadiliwa na baraza hilo; jambo linalopongezwa na Kiplagat kuwa hatua kubwa.


Nchi zingine zinazojadiliwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ni Chad, Sierra leone na Congo.