1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Maelfu wakimbilia kuvuka mpaka wa Ugiriki na Uturuki

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
2 Machi 2020

Uturuki imefungua mipaka yake kuwaruhusu wahamiaji na wakimbizi kutoka Syria wanaotafuta hifadhi katika nchi za Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3Yj0R
Türkei Provinz Hatay | Grenze zu Syrien | Cilvegözü Border Gate
Picha: DW/S. Görer

Maelfu ya wahamiaji wanajaribu kila njia ili waweze kuvuka mpaka wa eneo la magharibi mwa Uturuki na Ugiriki, baadhi yao wamefaulu kupita kwenye uzio wa seng'enge walioukata na wengine wamevuka kupitia kwenye mito baada ya Uturuki kufungua upande wake wa mpaka na kuwaruhusu wahamiaji na wakimbizi kuondoka nchini humo kwenda bara Ulaya. Hatua ya Uturuki ya kutangaza kuiweka mipaka yake wazi inalenga kuushinikiza Umoja wa Ulaya katika kuisaidia katika vita vyake na nchi jirani ya Syria.

Maelfu ya wanajeshi wa Uturuki wanaunga mkono vikosi vya waasi nchini Syria katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Idlib dhidi ya mashambulio ya vikosi vya serikali ya Syria vinayoungwa mkono na Urusi.

Mapambano katika eneo hilo la mwisho linaloshikiliwa na waasi wa Syria yamesababisha karibu raia milioni moja wakimbilie kwenye mpaka uliofungwa kati ya Syria na Uturuki, hali ambayo Uturuki inahofia kwamba idadi ya wakimbizi itaongezeka nchini humo ambapo tayari kuna wakimbizi milioni 3.5 kutoka Syria.Wakati hayo yakiendelea Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan anapanga kufanya safari ya siku moja kwenda Urusi Alhamisi wiki hii kukutana na mwenzake Vladimir Putin.

Wakimbizi wa Syria wakielekea kwenye mpaka wa Edirne kati ya Uturuki na Ugiriki
Wakimbizi wa Syria wakielekea kwenye mpaka wa Edirne kati ya Uturuki na UgirikiPicha: picture-alliance/NurPhoto/D. Cupolo

Juu ya matarajio ya Uturuki, mtaalam wa sera ya Mambo ya nje na Masuala ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Utamaduni cha mjini Istanbul. Bora Bayraktar amesema Uturuki inatarajia kuwa rais wa Urusi angeishawishi Syria kurudisha nyuma vikosi vyake kutoka kwenye maeneo waliopo wanajeshi wa Syria kwa sasa na ikiwa Urusi inataka kutekeleza malengo yake katika mkoa huo wa Idlib, na kufanikisha azma yake ya kimkakati kuwa mojawapo ya nchi zenye nguvu ulimwenguni inahitaji pia msaada wa Uturuki.

Erdogan alitarajiwa kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin baada ya askari 33 wa Uturuki kuuawa katika mashamulio ya ndege yaliyofanywa na wanajeshi wa Syria katika mkoa wa Idlib wiki iliyopita, hatua iliyosababisha Uturuki kulipiza mashambulio dhidi ya vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi.

Hapo jana Jumapili, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar alisema nchi yake ilianzisha operesheni mpya ya kijeshi dhidi ya vikosi vya Rais wa Syria Bashar al-Assad, na Syria iliifunga anga yake katika eneo la kaskazini-magharibi, haswa mkoa wa Idlib.

Mara kadhaa Uturuki na Urusi zimeshafanya mazungumzo ya kidiplomasia juu ya suala la Idlib, lakini hakuna mafanikio yaliyopatikana hata mara mmoja.

Vyanzo:/AP/RTRE/AFP