1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Taathira za ugomvi wa Ethiopia na Somalia Pembe ya Afrika

29 Januari 2024

Makubaliano ya Ethiopia kuhusu kukodisha bandari Somaliland yameighadhabisha serikali ya mjini Mogadishu na kuzusha wasiwasi kwamba hatua hiyo itavuruga zaidi utulivu wa eneo hilo la Pembe ya Afrika.

https://p.dw.com/p/4bn2t
Karte Somaliland EN
Ramani ya Somalia na jimbo lenye utawala wa ndani la Somaliland

Kulingana na makubaliano hayo yaliyosainiwa Januari mosi, Ethiopia ambayo ni taifa lisilokuwa na bandari yake, itakodisha takriban kilomita 20 ya sehemu ya bandari ya Berbera iliyoko eneo la Somaliland kwa miaka 50, kwa kubadilishana hisa katika makampuni ya serikali ya Ethiopia na vilevile uwezekano wa kutambua eneo hilo lenye mamlaka yake ya ndani kama taifa huru.

Somalia imesema mkataba huo ni kitendo cha uchokozi na imesisitiza kwamba itauzuia. Kwa upande wake, Ethiopia imeshikilia kuwa imeanzisha tu mpango wa kibiashara ili kushughulikia mahitaji yake ya kujipatai huduma za bahari.

Ethiopia, taifa lenye watu milioni 120 na hivyo kuwa la pili barani Afrika kwa idadi kubwa ya watu, hutegemea nchi jirani ya Djibouti kusafirisha asilimia 90 ya bidhaa zake kibiashara, hivyo kuigharimu zaidi ya dola bilioni 1.5 kila mwaka

Mnamo mwezi Oktoba, waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitoa hoja ya hadharani kuhusu hitaji la nchi yake kuwa na bandari. Aalitoa mfano wa Jenerali wa Ethiopia wa karne ya 19, ambaye aliitaja Bahari Nyekundu kuwa mpaka wa asili wa nchi hiyo.

Soma pia:  Rais wa Somalia afuta makubaliano ya Ethiopia, Somaliland

Ethiopia ilipoteza ufikiaji wa bahari mapema miaka ya 1990 wakati uliokuwa jimbo lake Eritrea, lilipojitenga na kuwa nchi kivyake kufuatia vita vya miongo mitatu. Msukumo wa Abiy wa kuirejesha unaonekana kupata uungwaji mkono mkubwa kisiasa.

Waziri Mkuu pia anataka kambi ya jeshi la wanamaji wa Ethiopia baharini. Wanajeshi wa kikosi hicho kilichoundwa upya katika miaka ya hivi karibuni, kwa sasa wanafanya mazoezi na mafunzo kwenye ziwa la ndani.

Serikali ya Mogadishu inachukulia Somaliland kama sehemu muhimu ya Somalia ingawa inayo mamlaka yake ya ndani.

Japo Somaliland ilijitangazia uhuru wake mwaka 1991, haijatambuliwa na nchi yoyote. Ikiwa Ethiopia itafanya hivyo, basi inaweza kuweka kielelezo kwa nchi nyingine kufuata.

Somalia imekataa pendekezo la Umoja wa Afrika la mazungumzo na Ethiopia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud wakisalimiana katika Ikulu ya Rais, mjini Mogadishu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud wakisalimiana katika Ikulu ya Rais, mjini Mogadishu.Picha: HASSAN ALI ELMI/AFP

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisaini sheria iliyokusudia kubatilisha mpango huo, na serikali yake ikakataa pendekezo la Umoja wa Afrika la mazungumzo na Ethiopia, likisema haitajadiliana juu ya uhuru wa nchi yake.

Kutokana na ukosefu wa utulivu nchini Ethiopia, Somalia na Sudan, pamoja na eneo la kimkakati la Pembe ya Afrika kote Bahari Nyekundu kutoka Ghuba, baadhi ya wachambuzi wanahofia mzozo huo ukiendelea, unaweza kutanuka zaidi.

Nchi zenye nguvu za Mashariki ya Kati, zikiwemo Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Uturuki na Qatar, zimekuwa zikipigania ushawishi katika kanda hiyo kwa kuendeleza uwekezaji wa kiuchumi, kufungua kambi za kijeshi na kuuza silaha.

Hadi sasa, hakuna nchi ambayo imeunga mkono hadharani mpango huo wa bandari.

Soma pia: Somalia: Wanajeshi walioko Eritrea kurejea nyumbani Disemba 

Jumuiya ya Kiarabu, ambayo Somalia ni mwanachama, ilithibitisha tena kuunga mkono uhuru wa Somalia juu ya Somaliland, kama walivyofanya Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Marekani.

Mnamo Jumapili, rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri, ambaye ana uhusiano baridi na Ethiopia kuhusiana na mzozo wa bwawa katika mto Nile alisema hataruhusu mtu yeyote kutishia Somalia.

Eritrea haijazungumzia mpango huo lakini muda mfupi tu baada baada ya mpango huo ulipotangazwa, rais wake Isaias Afwerki alimualika mwenzake Mohamud wa Somalia mjini Asmara.

Umoja wa Falme za Kiarabu, ambayo ni mshirika mkubwa wa Ethiopia na Somaliland na inasimamia bandari ya Berbera kupitia DP World inayoendeshwa na serikali, vilevile haijatoa kauli yake binafsi juu ya mpango huo tofauti na taarifa ya Jumuiya ya nchi za Kiarabu.