1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taiwan lazima iwe tayari kujilinda

28 Oktoba 2021

Waziri wa ulinzi wa Taiwan Chiu Kuo-cheng leo Alhamisi amesema lazima Taiwan iwe tayari kujilinda yenyewe na haiwezi kutegemea tu nchi nyingine kuisaidia iwapo China itafanya mashambulizi dhidi ya kisiwa hicho.

https://p.dw.com/p/42Hh0
Taiwanesischer Nationalfeiertag Millitär
Picha: Daniel Ceng Shou-Yi/ZUMA Press Wire/ZUMAPRESS/picture alliance

Awali rais wa Taiwan Tsai Ing-wen alisema kwamba ana imani na Marekani katika kuitetea Taiwan endapo China itachukua hatua yoyote. Soma Biden aapa kuilinda Taiwan endapo China itaivamia

Mzozo unaendelea kufukuta kati ya China na Taiwan na kufikia kiwango cha juu zaidi kushuhudiwa katika miongo kadhaa, huku China ikivunja rekodi ya kutuma ndege za kivita katika anga ya kimataifa karibu na kisiwa cha Taiwan katika kuendeleza kampeni ya vitisho vya kijeshi. 

Wizara ya ulinzi ya Taiwan imesema kwamba China itakuwa na uwezo kamili wa kuvamia kisiwa hicho ifikapo mwaka 2025. Waziri Chiu Kuo-cheng amesema "Nchi lazima ijitegemee yenyewe, na ikiwa marafiki wowote au vikundi vingine vinaweza kutusaidia, basi ni kama nilivyosema hapo awali, tunafurahi kuwa nayo, lakini hatuwezi kuitegemea kabisa."

China inadai kuwa Taiwan ni sehemu ya eneo lake, ingawa kisiwa hicho kilijitenga kutoka kwa utawala wa  kikomunisti mwaka 1949 baada ya miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Sera ya Marekani kwa Taiwan

Taiwanesischer Nationalfeiertag Präsident Tsai Ing-wen
Picha: Chiang Ying-ying/AP Photo/picture alliance

Wiki iliyopita, Rais wa Marekani Joe Biden alikwenda kinyume na sera ya muda mrefu ya Marekani kwa Taiwan aliposema kuwa Marekani imejitolea kulinda kisiwa hicho ikiwa China itakishambulia.

Marekani ina sera ya utata wa kimkakati kuelekea Taiwan, na imekuwa haieleweki kama itatetea kisiwa hicho wakati wa mashambulizi. Lakini pia nchi hiyo ina sera ya kuisadia Taiwankatika kujilinda wenyewe, ikiwa ni pamoja na kutoa silaha kama ilivyotangazwa katika Sheria ya Mahusiano ya Taiwan.

Huku haya yakijiri Beijing imepinga uhusiano wa kijeshi kati ya Washington na Taiwan, baada ya Rais Tsai Ing-wen kuthibitisha katika mahojiano na shirika la habari la CNN kwamba kuna idadi ndogo ya wanajeshi wa Marekani kisiwani humo kusaidia katika mafunzo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje China, Wang Wenbin amesema wanapinga aina yoyote ya ushirikiano rasmi na mawasiliano ya kijeshi kati ya Marekani na Taiwan, pia wanapinga uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya China, na majaribio ya kuchochea na kuzusha matatizo.

 

 

Vyanzo:AP/AFP