1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban kutangaza serikali yake licha ya uchumi kuyumba

Amina Mjahid
2 Septemba 2021

Watawala wa Kundi la Taliban wanapanga kuitangaza serikali yao mpya wakati uchumi wa Afghanistan ukihofiwa kuporomoka, ikiwa ni zaidi ya wiki 2 tangu Taliban ilipoudhibiti mji wa Kabul na kumaliza vita vya miaka 20

https://p.dw.com/p/3zoYG
Afghanistan Kabul - Taliban PK
Picha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Akiandika katika mtandao wa kijamii wa twitter, Ahmadullah Muttaqi mmoja wa maafisa wa kundi la Taliban, amesema wapo katika matayarisho ya kundaa ghafla ya kuitangaza serikali katika ikulu ya rais mjini Kabul, huku kituo binafsi cha habari cha Tolo kikithibitisha kuwa serikali hiyo itatangazwa hivi karibuni.

Uhalali na kutambuliwa kwa serikali hiyo na ulimwengu wa Kimataifa, wafadhili na wawekezaji ni muhimu kwa ukuaji uchumi wa Afghanistan, wakati taifa hilo likikabiliana na ukame na uharibifu mkubwa wa mali kutokana na miaka mingi ya vita viliyosababisha mauaji ya waafghan takriban 240,000.

soma zaidi: Biden atetea kuondoa vikosi nchini Afghanistan

Kiongozi Mkuu wa Taliban Haibatullah Akhundzada, anatarajiwa kuchukua madaraka ya juu zaidi katika baraza jipya la uongozi huku rais wa nchi akiwa chini yake.

Baraza la zamani la uongozi la Taliban ndilo lililoiwezesha kuiendesha nchi kwa misingi ya sheria kali za kidini kuanzia mwaka 1996 hadi walipoondolewa na wanajeshi wa Marekani mwaka 2001

Kwa sasa kundi hilo limejaribu kuionyesha dunia  sura tofauti na ile ya zamani tangu walipoiondoa serikali iliyoungwa mkono na Marekani. Limeahidi kulinda haki za binaadamu na kujizuwia kulipiza kisasi dhidi ya maadui zake.

kutambuliwa kwa serikali ya Taliban kutategemea na matendo yake

Afghanistan Hamid Karzai International Airport in Kabul
Baadhi ya wanachama wa Taliban Picha: REUTERS

Lakini Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine wanatilia shaka hatua za Taliban na kusema kuitambua serikali mpya na kuipa usaidizi wa kiuchumi kutategemea na matendo ya kundi hilo.

Huku hayo yakiarifiwa Umoja wa Mataifa umeonya kwamba unaweza mwezi huu kuishiwa na akiba ya  chakula inayoitumia kuwasaidia watu wa Afghanistan.

Umoja huo umesema hali hiyo inaweza kusababisha janga la njaa mbali na changamoto nyingine zinazozilikabili taifa hilo likiwa chini ya utawala waTaliban baada ya miongo miwili ya vita.

soma zaidi: Maroketi zaidi yaelekezwa Kabul

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu Afghanistan Ramiz Alakbarov amesema takriban watu milioni 38 wanaishi bila ya uhakika wa kupata mlo wa kila siku.

Mashirika ya kutetea haki za kibinaadamu kwa upande wao yameonya juu ya kutokea kwa mgogoro mkubwa wakati taifa likipitia ukame  na vita vilivyosababisha maelfu ya watu kuyatoroka makaazi yao.

Mashirika hayo yamesema Afghanistan kwa sasa inahitaji pesa na kundi la Taliban halionekani kufikia takriban bilioni 10 zinazozuiliwa nje ya nchi na benki kuu ya Afghanistan.

Chazo:reuters/ap/dpa