1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban na Magharibi waijadili hali nchini Afghanistan

Lilian Mtono
24 Januari 2022

Wanadiplomasia kutoka Taliban na mataifa ya magharibi wanakutana Oslo hii leo kwa mazungumzo kuhusu mzozo wa kibinaadamu na haki za binaadamu nchini Afghanistan na hususan haki za wanawake.

https://p.dw.com/p/45zqC
Afghanistan Wirtschaftskonferenz
Picha: Taliban Prime Minister Media Office/AP Photo/picture alliance

Tangu utawala wa Taliban urejee madarakani, haki za wanawake zimekuwa zikiminywa, kutokana na misimamo ya kundi hilo la Kiislamu lenye misimamo mikali.

Soma Zaidi: Afghanistan: Shule za sekondari zafunguliwa bila wasichana

Katika ziara ya kwanza barani Ulaya tangu kurejea kwa mamlaka ya Taliban nchini Afghanistan mwezi Agosti mwaka jana, serikali hiyo sasa inakutana na wawakilishi kutoka Marekani, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Italia, Umoja wa Ulaya na Norway.

Ujumbe wa Taliban unaongozwa na waziri wa mambo ya nje Amir Khan Muttaqi.

Mazungumzo hayo ya faragha, yaliyoratibiwa na Norway yanayofanyika nje kidogo ya mji wa Oslo, yanatarajiwa kujikita kwenye hali ya mzozo wa kibinaadamu ambayo imezorota mno tangu mwezi Agosti mwaka jana wakati wanamgambo hao waliporejea kwa kishindo baada ya miaka 20 tangu walipoondolewa madarakani.

Misaada ya kibinaadamu ilisitishwa na kusababisha kuzorota hata zaidi kwa mamilioni ya watu ambao tayari walikuwa wakikabiliwa na njaa, iliyosababishwa na ukame mkali na wa muda mrefu.

Norwegen Afghanistan-Gespräche mit den Taliban in Oslo
Wawakilishi wa Taliban walipowasili kwenye mazungumzo kuhusu mzozo wa kibinaadamu nchini Afghanistan yanyofanyika mjini Oslo.Picha: Terje Bendiksby/NTB/dpa/picture alliance

Jana Jumapili, katika siku ya kwanza ya ziara hiyo ya siku tatu mjini Oslo, Taliban walikutana na wajumbe wa vyama vya kiraia, ikiwa ni pamoja na wanaharakati wa haki za wanawake na waandishi wa habari kuzungumzia haki za binaadamu. Miongoni mwa wanaharakati hao wanawake anayehudhuria mazungumzo hayo Jamila Afghani ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "ulikuwa ni mkutano mzuri wa awali".

Wajumbe 15 wa Taliban ambao wote ni wanaume waliwasili Oslo jana Jumapili na miongoni mwao ni Anas Haqqani, kiongozi wa tawi linaloogopewa sana kutokana na kutumia mabavu la Haqqani Network linalohusishwa na baadhi ya mashambulizi ya kutisha nchini Afghanistan.

Mazungumzo haya hayamaanishi kutambuliwa kwa serikali ya Taliban.

Mwakilishi maalumu wa Marekani nchini Afghanistan Thomas West aliandika jana Jumapili kupitia ukurasa wa twitter kwamba "wakati tunapotafuta kushughulikia mzozo wa kibinaadamu kwa kushirikiana na washirika wetu, na mashirika ya misaada, tutaendelea kutumia diplomasia kuwaeleza Taliban kuhusiana na wasiwasi tulionao na maslahi yetu ya kudumu ndani ya Afghanistan iliyo imara, inayoheshimu haki na inayowajumuisha waAfghan wote."

Afghanistan verlorenes Baby nach langer Tortur zur Familie zurückgebracht
Raia wa Afghanistan wanakabiliwa na mzozo mkubwa wa kibinaadamu, ikiwa ni pamoja na njaa, hali ngumu ya uchumi na kitisho cha baridi kaliPicha: Ali Khara/REUTERS

Hakuna taifa ambalo limekwishaitambua serikali ya Taliban, na waziri wa mambo ya kigeni wa Norway Anniken Huitfeldt amesisitiza kwamba mazungumzo hayo "hayamaanishi kwamba wanaihalalisha ama kuitambua Taliban". "Lakini tunalazimika kuzungumza na mamlaka za taifa hilo. Hatutaruhusu hali ya kisiasa kuongoza taifa kuingia kwenye mzozo mbaya hata zaidi wa kibinaadamu", alisema Huitfedt Ijumaa iliyopita.

Lakini Taliban wenyewe wana matumaini kwamba mazungumzo hayo yatasaidia "kubadilisha ile hali ya vita....kuelekea kwenye hali ya amani", msemaji wa serikali ya Taliban Zabihullah Mujahid aliliambia shirika la habari la AFP jana Jumapili.

Pamoja na kusitishwa kwa misaada ya kimataifa, kumekuwa na ongezeko la kasi la ukosefu wa ajira na watumishi wa umma hawajalipwa mishahara kwa miezi kadhaa.

Soma Zaidi:Umoja wa Mataifa waitisha mkutano kuisadia Afghanistan 

Kitisho cha njaa kwa sasa ni dhahiri dhidi ya takriban watu milioni 23, ama asilimia 55 ya idadi jumla ya watu hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa ambao unasema unahitaji kiasi cha dola bilioni 4.4 kutoka kwa mataifa wafadhili kwa mwaka huu ili kushughulikia mzozo wa kibinaadamu nchini humo.

Mashirika: AFPE