1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yawasaka maadui nyumba kwa nyumba

Lilian Mtono
20 Agosti 2021

Ripoti ya shirika la kijasusi la Norway inasema wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan wanapita nyumba hadi nyumba kuwasaka watu ambao wanadaiwa kushirikiana na serikali iliyopita ya taifa hilo.

https://p.dw.com/p/3zDQQ
Afganistan | Taliban in Mazar-i-Sharif
Picha: Sputnik/dpa/picture alliance

Wanamgambo wa Taliban waliingia Kabul Jumapili iliyopita baada ya kuiangusha serikali ya rais Ashraf Ghani

Ripoti ya shirika la kijasusi la Norway la RHIPTO inatolewa wakati Wataliban wakijaribu kuonyesha kuwa na misimamo ya wastani tangu walipochukua udhibiti wa mji mkuu Kabul Jumapili iliyopita. Waliahidi msamaha kamili kwa wale wote walioshirikiana na serikali iliyokuwa ikiungwa mkono na mataifa ya Magharibi.

Soma Zaidi: Licha ya kukosolewa, Biden atetea uamuzi wa kuondoa vikosi Afghanistan

Ripoti hiyo imesema Taliban inaendelea kuwasaka watu binafsi na washirika wao kwenye serikali iliyopita na iwapo hawatafanikiwa, wataanza kuwakamata jamaa zao na kuwaadhibu. Ripoti hiyo imeongeza kuwa wanaolengwa zaidi ni waliokuwa na vyeo vikubwa kwenye jeshi la Afghanistan, polisi na mashirika ya kijasusi.

Kwa upande mwingine, maafisa wa vikosi vya kujihami vya NATO wamesema leo kwamba zaidi ya watu 18,000 wameikimbia Kabul tangu Taliban ilipochukua udhibiti Jumapili iliyopita na kuahidi kuongeza kasi ya kuwahamisha huku wakiendelea kukabiliwa na ukosoaji wa namna walivyoshughulikia suala hilo.

Soma Zaidi: Licha ya ahadi ya Taliban kutolipiza kisasi, maelfu waondoka

Afghanistan Kabul | Straße zum Flughafen
Raia wa Afghanistan wakiwa wamekaa pembezoni mwa barabara wakisubiri kuchukuliwa na ndege ya kijeshi ya Marekani Picha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Hata hivyo Taliban wenyewe wamewaomba viongozi wa dini kabla ya swala maalum ya Ijumaa kuwahimiza watu kutoondoka Afghanistan wakati uwanja wa ndege ukiwa umegubikwa na ghasia.

Taliban yaahidi kuunda serikali shirikishi.

Huku hayo yakiendelea, msemaji wa Taliban kwenye ofisi ya kisiasa iliyoko Qatar, Suhail Shaheen amesema jana kwamba mazungumzo ya kuunda serikali mpya na shirikishi yanaendelea. Amesema alipozungumza na mtangazaji wa shirika la habari la China la CMG, Tian Wei kwamba serikali hiyo haitahusisha Wataliban tu, bali pia wanasiasa wengine wa Afghanistan.

"Sisi ni Emirati ya Kiislamu ya Afghanistan, na ndio maana tunaunda serikali jumuishi ya Kiislamu ya Afghanistan baada ya mashauriano na viongozi wa juu. Hadi sasa hayo ndio makubaliano na ndio maana mazungumzo au mashauriano yanaendelea kwa ajili ya lengo hilo." alisema Shaheen.

Ameongeza muundo wa serikali mpya utatangazwa hivi karibuni.

Nchini Ugiriki, waziri mkuu Kyriakos Mitsotakis anatarajiwa kujadiliana na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuhusiana na hali nchini Afghanistan hii leo wakati Ugiriki ikihofia kitisho cha wahamiaji wengi kuingia nchini humo kama ilivyokuwa mwaka 2015. Mitsotakis na Erdogan watazungumza kwa njia ya simu baadae, imesema ofisi ya waziri mkuu wa Ugiriki.

Lakini taarifa za kusikitisha zinasema, wanamgambo hao wa Taliban waliokuwa wakimtafuta mwandishi wa habari wa DW wamemuua ndugu ya mwandishi huyo na kuwajeruhi vibaya wengine, hii ikiwa ni kulingana na shirika hilo la habari la umma. DW limesema walichukua maamuzi hayo baada ya kumsaka na kumkosa kwa kuwa sasa anafanya kazi Ujerumani. Ndugu zake wengine wamekimbia. 

Mashirika: RTRE/DPAE/APE/DW