1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamasha la maonyesho ya utalii Zanzibar

Salma Said 17 Oktoba 2018

Tamasha la maonyesho ya utalii linafanyika Zanzibar kwa lengo la kukuza uchumi. Sherehe, maonesho ya bidhaa na maeneo ya vivutio yanaoneshwa kwa wageni na wenyeji zaidi ya 1000.

https://p.dw.com/p/36hCH
Tansania | Politiker besuchen die erste Tourismusausstellung in Sansibar
Picha: DW/S. Said

Kwa mara ya kwanza Zanzibar imeanza kufanya Tamasha la Maonesho ya Utalii ikiwa ni jitihada za kuimarisha uchumi, wakati huu ambapo nchi mbalimbali Duniani zipo katika kuimarisha Utalii ili kutoa mchango zaidi katika kukuza Uchumi. Tamasha hilo la wiki moja limefunguliwa Jumatano katika viwanja na fukwe ya hoteli mpya ya kifahari ya Verde ambapo sherehe na maonesho ya bidhaa na maeneo ya vivutio vinaoneshwa kwa wageni na wenyeji zaidi ya 1000.

Zanzibar ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitegemea Karafuu kama chanzo kikuu cha mapato yake, katika miaka ya hivi karibuni utalii umechukuwa nafasi ya kwanza ambapo zaidi ya asilimia 80 ya Fedha za kigeni katika hazina ya Serikali zinatokana na utalii.

Kila Mwaka watalii zaidi ya laki tatu wanatembelea Zanzibar, Lakini wakati Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Shein akifunguwa Tamasha hilo la utalii ambalo liliwashirikisha wageni na wanyeji zaidi ya 1000, Alisema Tamasha ni miongoni mwa mikakati ya kuongeza Idadi ya watalii kufikia laki tano ifikapo mwaka wa 2020.

Mipango ya serikali kuimarisha utalii

Kila mwaka Tanzania hupokea zaidi ya watalii 300,000
Kila mwaka Tanzania hupokea zaidi ya watalii 300,000Picha: DW/S. Said

Aidha alitaja mipango madhubuti ya serikali katika kuimarisha sekta ya utalii ikiwemo kuwepo kwa hali ya utulivu na amani, kuimarisha sekta ya utalii, ikifuatiwa na kuendelea kunawiri kwa hali ya uchumi ambapo mwaka jana 2017, utalii ulikuwa kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na asilimia 6.8 kwa mwaka 2016.

Jambo jengine ni kuongezeka kwa kipato cha wananchi, jambo ambalo linawapa uwezo zaidi wa kununua vitu wanavyovipenda kwa lengo la kuimarisha zaidi hali zao za maisha, fursa ya wawekezaji kumiliki asilimia 100 ya miradi wanayowekeza pamoja na ruhusa ya kuajiri wataalamu, pale ikithibitika kwamba wameshindwa kupata wataalamu wazalendo pamoja na urahisi wa wawekezaji na wafanyakazi wa kigeni kupata vibali vya kazi na ukaazi.

Jengine ambalo limetajwa ni kuwepo na utawala na usimamizi mzuri wa fedha na ulipaji wa kodi, Fursa kubwa ya masoko kwa bidhaa na huduma zinazotolewa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar Shein asema tamasha ni miongoni mwa mikakati ya kuongeza Idadi ya watalii kufikia laki tano ifikapo mwaka wa 2020.
Rais wa Zanzibar Shein asema tamasha ni miongoni mwa mikakati ya kuongeza Idadi ya watalii kufikia laki tano ifikapo mwaka wa 2020.Picha: DW/S. Said

Katibu Mkuu wa wizara ya habari utalii na mambo ya kale, Khadija Bakari amesema kwamba kupitia tamasha hili, sekta ya utalii itaimarika zaidi.

Uimarishaji wa utalii wa ndani

Mikakati mingine ni kuimarisha miundombinu na vivutio zaidi mfano utalii wa utamaduni, pamoja na utalii wa ndani ambapo wananchi wanashajiishwa kutembelea Maeneo ya utalii.

Zaidi ya miaka 30 Zanzibar ilianza kuimarisha sekta yake ya utalii na kupata mafanikio makubwa ambapo leo Serikali imetambua mchango wa wadau katika kuimarisha utalii wa Zanzibar ambapo jumla ya wadau 24 wageni na wenyeji wamepatiwa vyeti maalumu vya shukrani akiwemo mwekezaji mkongwe kabisa wa hoteli ya kitalii ambaye ni mwana mapinduzi Ali Sultan Issa.

Katika maonesho haya kumefanyika mashindano ya ubora katika huduma ya utalii kupitia sekta ya hoteli mikahawa, wapishi, utunzaji mazingira, utembezaji utalii bora ambapo jumla ya wadau 20 wengine watapewa tunzo maalum wakati ufungaji wa tamasha hilo ifikapo Oktoba 20 mwaka huu.

Tamasha hilo pia linafanyika siku chache tangu dunia kuadhimisha siku ya kimataifa ya utalii ambao kauli mbiu ya mwaka huu ni "Umuhimu wa Teknolojia ya Dijitali katika Utalii Endelevu."