1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha ACT Wazalendo kinapanga safu mpya

5 Machi 2024

Chama cha upinzani nchini Tanzania ACT Wazalendo kinapanga upya safu yake ya uongozi kwa kufanya uchaguzi mkuu huku kiongozi wa muda mrefu wa chama hicho, Zitto Kabwe akiachia nafasi yake.

https://p.dw.com/p/4dB92
Tanzania Dar es Salaam | Mkutano wa mageuzi ya uchaguzi katika maandalizi ya chaguzi za mitaa na bunge
Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Salumu Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chedema na Bakari Machumu, Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications waliohudhuria mkutano wa Vyama vya Siasa jijini Dar es Salaam, Tanzania.Picha: Florence Majani/DW

Uchaguzi huo unatazamwa kama hatua mojawapo kwa vyama vya upinzani nchini humo kuanza kujipanga kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu wa mwakani.

Uchaguzi huu ambao unafanyika kama sehemu ya matakwa ya katiba yake, unatazamiwa kuwasogeza katika nafasi za juu za uongozi kwa baadhi ya watendaji wake, ingawa karibu ya wote waliojitokeza kuwania nafasi wamekuwa ndani ya uongozi wa chama hicho.

Zitto Kabwe ambaye ni sehemu ya waasisi wa chama hicho, anaondoka kwenye nafasi yake kama kiongozi wa chama akifanya hicho kutimiza matakwa ya katiba baada ya kukaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka kumi.

Zitto Kabwe anarejea kuwania ubunge

Tanzania Africa Zitto Kabwe
Zitto Kabwe, Kiongozi wa Upinzani Tanzania wa chama cha Alliance for Change & Transparency ACT anaemaliza muda wake.Picha: privat

Tayari mwenyewe amedokeza shabaha yake ya kurejea jimboni kwake, Kigoma atakakopeperusha bendera ya chama chake katika uchaguzi mkuu wa mwakani. Nafasi yake inawaniwa na wagombea wawili akiwemo makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania bara, Doroth Semu anayepambana na mwanasiasa mwingine, Mbarala Maharagande.

Makamu wa kwanza wa Rais katika serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Othman Masoud Othman anatazamiwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho, baada ya aliyekuwa mpinzani wake Juma Duni Haji kujitoa katika dakika za lala salama.

Wajumbe wamekusanyika katika eneo la mlimani City wanakoshirki mkutano mkuu wa chama ambao baadaye wataamua hatma ya chama chao kwa kuwachagua viongozi. Mkutano huo mkuu umewaleta pamoja wajumbe kutoka kila kona ya nchi huku pia ukiwaalika viongozi wa vyama kutoka kambi nyingine.

Mpinzani kutoka Burundi  Aghanton Rwasa ahimza ACT kujipanga kwa uchaguzi

Akizungumza kwenye mkutano huo, kiongozi wa chama CNL kutoka Burundi, Aghaton Rwasa aliwapa shime viongozi wa chama hicho kuutupia macho uchaguzi ujao akiwataka kujipanga kisanyansi.

Wakati akitoa nasaha zake kwenye mkutano huo unaoendelea, Makamu Mwenyekirti wa chama tawala CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana alitaja kwamba ACT Wazalendo ni chama kinachopiga hatua kusonga mbele.

Soma zaidi:Uchaguzi mdogo Zanzibar unaakisi ushindani wa kisiasa?

Mbali na hayo yanayoendelea kwa chama hicho, nacho chama kingine cha upinzani Chadema viongozi wake wakuu wanaanza kukutana leo  (05.03.2024)  kutathmini maandamano yake yaliyofanyika hivi karibini pamoja na kupanga mikakati ya kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na ule ujao.

DW: Dar es Salaam