1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania Sheria ya Udhibiti wa Manunuzi Serikalini sasa Inafanya kazi.

Christopher Buke25 Mei 2007

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari inasema ni utaratibu mzuri.

https://p.dw.com/p/CHkn

Udhibiti wa fedha na rasilmali za serikali hivi sasa ni suala linalozungumzwa sana nchini Tanzania. Iwe kwa wanasiasa, vyama vya kijamii mashirika ya Umma, vyama vya siasa lakini hata kwa watu wa kawaida.

Bila shaka kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo inatokana na kuwekwa wazi ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania aliyoitoa hivi karibuni ikionyesha takliban shilingi bilioni 273 ziliyeyuka au hazina maelezo yanayokidhi katika kipindi cha mwaka jana.

Ripoti hiyo inafafanua kuwa sehemu kubwa ya fedha hii inatoweka wakati wa manunuzi na malipo.

Lakini kwa upande mwingine ripoti hiyo imeipa nguvu sheria na Taasisi ya udhibiti wa Ununuzi wa mali za serikali PPRA kwa vile sasa unaonekana umuhimu wa kuwa macho mno na jinsi serikali na taasisi zake zinavyotumia fedha za taifa.

Sasa hivi viongozi wa mashirika, taasisi za serikali wanawapa semina maafisa wao hasa walio katika idara za ununuzi na ugavi jinsi ya kufuata utaratibu huu wa PPRA.

Mojawapo ya mashirika hayo ni shirika kubwa kabisa nchini Tanzania ambalo ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania.

Akizungumza na Deutsche Welle nje ya ukumbi wa mkutano inapofanyikia semina hiyo Bwana Hassan Kyomile ambaye ni Meneja Ununuzi na Ugave katika mamlaka hiyo alisema shirika hilo lilikuwa na utaraibu mzuri hata kabla ya kutolewa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Sheria hii mpya ya Public Procurements Act inazitaka sekta na taasisi zote za serikali kupeleka mipango ya manunuzi ya idara hizo mapema kabla ya kuanza ununuzi wa mahitaji husika.

Afisa huyo wa Bandari anasisitiza kuwa Mamlaka ya Bandari imekuwa ikifanya kazi kwa misingi ya kitaaluma na kwa mwongozo wa mashirika ya kimataifa IMF na Benki ya Dunia.

“Kwa hiyo tulikuwa tukifanya manunuzi yetu na kupanga kulingana na vyombo vilivyokuwepo nyuma na mara nyingi tulikuwa tunafuata sheria za Benki ya Dunia na shirika la fedha la dunia IMF” anasema Bwana Kyomile na kuongeza

“tulikuwa tunafuata taratibu zao. Ukiangalia sheria yetu ya sasa hivi masuala mengi sana yamezingatia sheria za World Bank na IMF kwa hiyo kiutekelezaji hatuna tofauti sana ila matakwa mengine sasa yanayokuja kwa mfano kutakiwa kupeleka hiyo mipango kwenye Public Procurement Regulatory Authority huko nyuma haikuwepo”.

Lakini baadhi wana mashaka kuwa utaratibu huu mpya unaweza kusababisha ucheleweshaji, au urasimu kutokana na kuwa ikiwa shirika kwa mfano lina hitaji la kununua vifaa ambavyo viliwezeshe kuboresha utendaji na kwa haraka lazima kwanza lipeleke maelezo katika bodi hiyo.

Bwana Kyomile kwa upande wake anadhani kwa Bandari sio tatizo akisema “kule tunakwenda kuomba idhini ila tunawataarifu kusudi wao baadae katika kukagua utekelezaji wawe na mahala pa kuanzia kuanza kuhakiki kwamba ulipanga kuanza kufanya hivi lakini mbona hujafanya”.

Kwa upande wake anaisifu sheria hii kuwa japo baadhi wanaiona kuwa inaweza kuleta urasimu lakini ni sheria inayoyawezesha mashirika kuweka mipango yao vizuri ya muda mrefu na muda mfupi.

Anasema sheria hiyo imechambua aina zote za mahitaji muhimu na kuainisha namna gani yashughulikiwe “Kuna mahitaji ya kawaida yana namna ya kuyashughulikia mpaka dharula imewekwa mle kuna namna ya kushughulikia dharura”.

Kwa upande wake Dk. Ombeni Onesmo Mbwambo ambaye ni daktari Mkuu wa Usimamizi wa Bandari Tanzania ambaye ni mshiriki wa mkutano huo anadhani sheria hii itaondoa aina fulani ya mizengwe iliyokuwa ikijitokeza katika baadhi ya mashirika.

“kama taratibu zitatumika vizuri hasa katika mambo ya planning yatapunguza sana mambo ya ucheleweshaji wa manunuzi, itapunguza watu kufanya vitu kidharura na itapunguza vile vile matumizi mabaya ya fedha za umma”.

Naye Bi Nusra Othman anasema kuwa haoni kwa nini watu wanastushwa na sheria hii kwani imekuwepo tangu mwaka 2004 ilipotambulishwa na kuwa tangu wakati huo idara na taasisi mbalimbali za serikali zilipaswa kujiandaa ili kuendana na sheria hiyo.

Mwisho.