1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania:upinzani waapa kuendelea kudai mabadiliko ya katiba

George Njogopa27 Julai 2021

Vyama vya upinzani Tanzania vimesisitiza kuwa licha ya Mbowe kufunguliwa mashtaka havitarudi nyuma katika vuguvugu la kudai mabadiliko ya katiba mpya.

https://p.dw.com/p/3y7TK
Tansania Opposition Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/AFP/Getty Images

Mwenyekiti Mbowe ambaye jana alifikishwa kimya kimya katika mahakama ya mkazi kisutu na kusomewa mashtaka yanayohusiana na kula njama za kuendesha vitendo vya ugaidi na utakatishaji wa fedha, amewafanya karibu wanasiasa wote wa upinzani kulilaani tukio hilo ambalo chama chake pia kimeelezea masikitiko yake.

Vikionekana kuwa na msimamo unaofafa, vyama hivyo ambavyo vimekuwa vikiimba wimbo wa kutaka katiba mpya kwa kipindi cha miaka mingi, mbali ya kulaani vikali lakini pia vinataka kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa yanayosaidia kulivusha taifa kutoka lilipo na kuingia katika enzi yenye kuaminiana kisiasa.

Upi muelekeo wa chama cha Chadema ?

Akiwa katika jambo hilo, Mkurugenzi wa habari, uenezi na mahusiano na umma, Injinia Mohamed Ngulangwa ameeleza kwamba, mjadala wa katiba unapaswa kuwa huru kwa vile unawakilisha utashi wa wananchi.

Ameonyesha kutovutiwa na namna mwenyekiti Mbowe alivyokumbwa na masaibu hayo wakati akiwa katika jukwaa la kuhimiza mabadiliko ya katiba mpya.

''Tunalaami hayo yanayoendelea kufanyika kama lengo lake ni kukwamisha kupatikana kwa katiba mpya au kukwamisha michakato ya kidemokrasia nadani ya ardhi ya Tanzania. Na tunasema tuache mara moja mambo haya, lazima vyama vikae pamoja kwa ajili ya kuangalia mustakbali wa taifa hili.'',alisema Ngulangwa.

''Tumeamini kabisa kwamba katiba mpya ni takwa la wananchi wote''

Vuguvugu la kudai mabadiliko ya katiba kuendelea na mchakato wake
Vuguvugu la kudai mabadiliko ya katiba kuendelea na mchakato wakePicha: DW/S. Khamis

Nacho chama cha ACT Wazalendo hakijakwenda mbali zaidi juu ya hoja kama hiyo na Naibu katibu mkuu anayehusika na masula ya uenezi, Janeth Rithe anasema safari ya kudai katiba mkuu hawezi kusema inaishia njiani kutokana na hayo yaliyojitokeza kwa Chadema.

''Jambo hili la katiba mpya haliwezi kurudi nyuma kwa sababu ya viongozi kukamatwa.Tumeamini kabisa kwamba katiba mpya ni takwa la wananchi wote wa Tanzania.'' alisema Rithe.

Duru za kuaminika zinaeleza kuwa Kamati Kuu ya Chadema imepanga kufanya kikao cha dharura leo Jumanne kujadili kile kilichojitokeza kwa mwenyekiti Mbowe na huenda kikatoa msimamo wake baada ya kumalizika kikao hicho.

Akizungumza katika jukwaa moja la mtandaoni lilipeperushwa hewani jana usiku, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Goodbless Lema alidai kuwa chama hicho bado kinajihisi kipo imara na kitaendelea na kile alichokisema vuguvugu la kupigania katiba mpya.

Nao baadhi ya wanachama wa chama hicho wanaunda baraza la wanawake,BAVICHA. Jana walipiga hodi katika ofisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa wakiwa na mabango mikononi kuelezea kilio chao kutokana na yale yaliyomfika Mbowe.

Mwenyekiti huyo ambaye alikamatwa wiki iliyopita jijini Mwanza na kisha kusafirishwa hadi Dar es salaam wakati akiwa katika maandalizi ya kuliongoza kongamano la ndani kuhusiana na katiba mpya, anatarajiwa kufikishwa Mahakama Kuu mwezi ujao kuyakabili mashtaka yake.