1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yawakamata watu 104 kwa kutaka kujiunga na waasi

Caro Robi
22 Oktoba 2018

Mkuu wa Polisi wa Tanzania Simon Sirro amesema majeshi ya polisi yameanzisha operesheni dhidi ya wahalifu na watu 104 wanaoshukiwa kupanga kuanzisha ngome yao katika taifa jirani la Msumbiji wamekamatwa.

https://p.dw.com/p/36w7k
Simon Sirro  Polizeichef Dar es Salaam
Picha: DW/H.Bihoga

Polisi nchini Tanzania wamewakamata watu 104 wanaoshukiwa kuwa waasi wanaopanga kuanzisha ngome yao katika taifa jirani la Msumbiji ambako watu kadhaa wameauwa katika mashambulizi ya itikadi kali za Kiislamu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mkuu wa Polisi wa Tanzania Inspekta Jenerali Simon Sirro amesema majeshi ya polisi yameanzisha operesheni dhidi ya wahalifu mashariki na kusini mwa nchi na baadhi ya washukiwa walikamatwa, wengine walikufa na wengine walitoroka.

Sirro amesema washukiwa waliokamatwa walipohojiwa wamesema walikuwa wanakwenda Msumbiji kujiunga na makundi ya wapiganaji wenye misimamo mikali.

Mshambulizi takriban 40 yamefanyika tangu Oktoba mwaka jana katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji ambalo liko mpakani na Tanzania. Zaidi ya watu 100 wameuawa katika mashambulizi hayo.