1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko kubwa mpakani mwa Iran na Irak

Zainab Aziz
13 Novemba 2017

Watu zaidi ya 300 wamekufa kutokana na tetemeko la ardhi lililofikia kiwango cha 7.3 kwenye eneo la mpakani baina ya Iran na Irak. Watu wengine 3000 wamejeruhiwa. Uturuki, Japan na Costa Rica pia zimeguswa.

https://p.dw.com/p/2nVdv
Iran Erdbeben
Picha: Reuters/Tasnim News Agency

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na maafisa wa Iran watu hao wamekufa katika eneo ambalo liko mpakani mwa nchi hizo mbili baada ya eneo hilo kukumbwa na tetemeko kubwa hapo jana usiku.  Maafisa wa uokozi wamesema wanahofia kuwa huenda idadi ya watu waliokufa ikaongezeka. Zaidi ya watu 60 walikuwa katika mji wa Sarpol e Zahab ulio umbali wa kilomita 15 karibu na mpaka wa Iran na Irak. Wakati huo huo wizara ya mambo ya ndani ya Iran amesema helikopta hazikuweza kupaa angani wakati wa usiku ili kuyafikia maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi hali ambayo ilichangia matatizo zaidi lakini hadi sasa shughuli za uokoaji zinaendelea. 
Naibu gavana wa jimbo la Kermanshah amesema kambi tatu za msaada zimewekwa. Miji ilioathirika zaidi kwa upande wa Iran ni ya Kermanshah na Azgaleh iliyopo kilomita 40 kaskazini magharibi mwa Iran. Kwa upande wa Irak jimbo la Sulaimaniyah ambalo ni eneo la Wakurdi ndio limefikwa na maafa hayo.Shirika la utafiti wa Jiolojia la Marekani limesema kitovu cha tetemeko hilo lililofikia nguvu ya kiwango cha 7.3 katika kipimo cha Richter kilikuwa umbali wa kilomita 30 kutoka mji wa Halabja uliopo mashariki mwa Irak na pia karibu na mji wa Erbil. Matetemeko mawili madogo yametokea baada ya tetemeko hilo kubwa la jana usiku. La kwanza lililofikia kiwango cha 4.5 lilitokea muda mfupi tu baada ya tetemeko hilo kubwa na la pili lenye nguvu ya 4.7 limetokea mapema leo.  Maafisa wa Irak wamesema hali ni mbaya mno na yametokea madhara makubwa, majengo yameharibiwa sana na huduma ya umeme imekatika katika vijiji kadhaa.   Familia nyingi zimelala nje ya nyumba zao kwa hofu ya kutokea kwa tetemeko jingine. Tetemeko hilo lilitikisa hadi kusini mashariki mwa Uturuki.
Wakati huo huo.

Iran Erdbeben
Majeruhi kadhaa wa tetemeko la ardhi wapokea matibabuPicha: Reuters/Tasnim News Agency
Iran Erdbeben
Wahanga wa tetemeko la ardhiPicha: Reuters/Tasnim News Agency

Japan imeripoti kwamba tetemeko lililofikia nguvu ya 5.8 lilikumba pwani ya mashariki mwa nchi hiyo saa chache kabla ya tetemeko la mpakani mwa Iran na Irak kutokea. Vilevile nchini Costa Rica kulitokea pia tetemeko lenye nguvu ya 6.5 ambalo liliutikisa mji wake mkuu wa San Jose.

Watu wawili wamefariki kutokana na mshtuko wa moyo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na msemaji wa wizara ya Usalama wa umma nchini humo. Wizara ya afya ya Uturuki imesema iko tayari kutoa msaada katika eneo la kaskazini mwa Irak na shirika la kimataifa la uokoaji IRC limesema liko katika hali ya tahadhari iwapo msaada utahitajika wakati wowote.
Mwandishi: Zainab Aziz APE/DPAE/dw.com/p/2nV75
Mhariri: Josephat Charo