1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tiangaye waziri mkuu mpya Afrika ya Kati

18 Januari 2013

Kufuatia makubaliano ya amani kati ya waasi na serikali, Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amemteua Nicolas Tiangaye kutoka upinzani kuwa waziri mkuu mpya ili kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

https://p.dw.com/p/17Mk9
Rais Francoise Bozize (kulia) akipeana mkono na kiongozi wa waasi wa Seleka, Michel Djotodia.
Rais Francoise Bozize (kulia) akipeana mkono na kiongozi wa waasi wa Seleka, Michel Djotodia.Picha: dapd

Nicholas Tiangaye, mwanasheria na kiongozi wa chama cha mageuzi ya kijamaa amepata ridhaa kutoka kwa makundi ya waasi kufuatia mazungumzo ya amani yaliyofanyika katika mji mkuu wa Gabon, Libraville.

Redio ya serikali ya nchi hiyo ilitangaza kwamba kwa mujibu wa sheria, rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amemteua Tiangaye kuwa waziri mkuu.

Waziri huyo mkuu mpya sasa atachukua jukumu la kuwachagua mawaziri watakaoshirki serikali ya umoja wa kitaifa na kuipeleka nchi hiyo kwenye uchaguzi wa bunge miezi 12 ijayo ili kuchukua nafasi ya bunge la sasa lililo na wajumbe wengi wanaomuunga mkono rais pekee.

Waasi wakubali kuacha mapigano

Katika mazungumzo, waasi walikubali kusitisha mapigano na pia kumwachia Rais Bozize amalizie muhula wake madarakani hadi mwaka 2016.

Kikao cha upatanishi kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na waasi wa Seleka nchini Gabon.
Kikao cha upatanishi kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na waasi wa Seleka nchini Gabon.Picha: dapd

Akizungumza na shirika la habari la Reuters mara baada ya kutangazwa, Tiangaye alisema ameridhishwa na hatua ya kuwa sehemu ya matumaini mapya ya hatima ya Jamhuri ya Afrika ya kati katika kuimarisha amani.

Muungano wa makundi matano ya waasi, Seleka, mwezi uliopita yaliuzingira mji mkuu, Bangui, na kumtaka Rais Bozize ajiuzulu. Makundi yote yanamtaja Tiangaye kama mtu anayechukia rushwa.

"Ni mtu mwenye ujasiri, mwenye kumbukumbu ya kufanya mambo kwa umakini mkubwa, ni mtu tunayemuheshimu sana," alisema Martin Ziguele mjumbe wa waasi akiungwa mkono na msemaji wa kundi hilo, Eric Massi.

Tiangaye kutowania urais

Waziri Mkuu Tiangaye hatakuwa tena na matumaini ya kuwania urais wa nchi hiyo, kwani kwa mujibu wa makubaliano ya amani kati ya makundi ya upinzani, waasi na serikali yaliyopelekea kuchaguliwa kwake yanamzuia Waziri Mkuu kuwania kiti cha urais.

Lakini kuhusu hilo, mwenyewe anasema si lazima yeye kuwa rais na mtu yeyote anaweza kuwa rais, na anachotaka yeye ni kuweka msingi wa demokrasia katika taifa hilo.

Alizaliwa mnamo mwaka 1956 kaskazini magharibi ya mji wa Bocaranga. Baba yake alikuwa muuguzi, na alipata masomo yake mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui, na Ufaransa na kumaliza mwaka 1980.

Alijipatia umashuhuri mnamo mwaka 1986 pale alipomtetea mahakamani mfalme wa zamani wa nchi hiyo, Jean -Bedel Bokassa.

Mnamo mwaka 1989 alijipatia umaarufu kwa mara nyengine alipoamua kumtetea rais aliyepo sasa, Francois Bozize, pale aliposhitakiwa kwa njama dhidi ya aliyekuwa rais wa wakati huo, Andre Kolingba.

Amekuwa akiliongoza baraza la mpito la upinzani, na ni miongoni mwa washiriki katika uandaaji wa katiba ya sasa ya nchi hiyo ya mwaka 2004, iliyopatikana kwa kura ya maoni ambayo inatamka kuwa rais hatawania nafasi hiyo kwa zaidi ya vipindi viwili.

Mwandishi: Khatib Mjaja/AFPE/REUTERS
Mhariri: Josephat Charo