1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TPLF yaondolewa katika orodha ya makundi ya kigaidi Ethiopia

Amina Mjahid
22 Machi 2023

Wabunge wa Ethiopia wamekiondoa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF katika orodha ya makundi ya kigaidi, ikiwa ni zaidi ya miezi 4 baada ya makubaliano ya amani kuumaliza mgogoro uliopelekea maelfu ya watu kuuwawa

https://p.dw.com/p/4P4Oo
Äthiopien Tigray | Waffenübergabe der Rebellen an Armee
Picha: Ethiopian Broadcasting Corporation

Maamuzi yaliyochukuliwa hii leo yanaonyesha mahusiano yaliyoimarika kati ya maafisa wa serikali ya shirikisho na wale wa jimbo la Tigray, hatua inayotoa uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya mpito.

Kulingana na shirika la habari la serikali, wabunge wengi miongoni mwa wabunge 547 wa bunge la Ethiopia, walipiga kura kikiondoa chama hicho katika orodha hiyo. Wabunge 61 tu ndio waliopinga na watano kutoshiriki kabisa mchakato huo. TPLF iliingizwa rasmi katika orodha ya makundi ya magaidi mwaka 2012.

Ethiopia na TPLF kuunda chombo cha kusimamia makubaliano ya amani

Kindeya Gebrehiwot, afisa mkuu wa chama cha TPLF ameliambia shirika la habari la The Associated Press kwamba hatua iliyochukuliwa ya kukiondoa katika orodha ya makundi ya kigadi ni hatua muhimu inayosogeza mbele makubaliano ya amani.

Kuondolewa kwa chama cha TPLF katika orodha hiyo, ni miongoni mwa masharti ya chama hicho ili kishiriki kikamilifu kwenye serikali ya mpito.

Waasi wa Tigray waanza kuzisalimisha silaha zao nzito

Chama cha TPLF kilijiingiza katika siasa za Ethiopia kwa zaidi ya miongo mitatu kabla ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuchukua uongozi mwaka 2018. Baadae mwaka 2020 mgogoro ukaanza ndani ya jimbo la Tigray.

Serikali ya Ethiopia iliituhumu TPLF kuanzisha mgogoro kwa kushambulia kambi ya jeshi katika jimbo la Tigray, huku TPLF nao wakiishutumu serikali hiyo ya shirikisho iliyokuwa tayari imejitayarisha kuwashambulia.

Makubaliano ya amani yaleta muelekeo mpya wa kisiasa Ethiopia

Äthiopien Friedensabkommen Tigray
Muakilishi wa serikali ya Ethiopia Redwan Hussein na Muakilishi wa TPLF Getachew Reda wakitia saini makubaliano ya amani nchini Afrika Kusini Picha: PHILL MAGAKOE/AFP/Getty Images

Serikali ya Ethiopia na chama cha TPLF walitia saini nchini Afrika Kusini mwezi Novemba makubaliano ya kusitisha vita na kuruhusu msaada kuingizwa Tigray pamoja na wapiganaji wa TPLF kuweka chini silaha na kurudishwa tena kwa mamlaka ya shirikisho katika jimbo hilo la Tigray.

Marekani yasema uhalifu wa kivita ulifanywa katika vita vya Tigray nchini Ethiopia

Makubaliano hayo pia yalifungua njia ya kurejeshwa kwa mawasiliano, huduma za benki na huduma nyengine muhimu zilizokuwa zimesitishwa katika jimbo la Tigray lililo na idadi ya watu milioni 5. Ethiopia kwa sasa inahitaji takriban dola bilioni 20 ili kulijenga upya taifa hilo baada ya miaka miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mapema wiki hii, Marekani ilisema kuwa imegundua kwamba pande zote katika mzozo wa Ethiopia, zilitekeleza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu.

Blinken aiomba Ethiopia kuimarisha amani baada ya vita

Katika tamko lake Marekani ilizitaja hasa serikali ya Ethiopia, Eritrea na vikosi vya wanajeshi kutoka mkoa wa Amhara kutekeleza uhalifu huo bila kuwataja moja kwa moja wapiganaji wa Tigray.

Lakini muda mfupi baada ya tangazo hilo kutoka Marekani, wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia ilikanusha vikali tamko hilo ikiikosoa taarifa ya Marekani na kusema ni ya kibaguzi na inayoegemea upande mmoja.

Chanzo: ap