1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Transparency International yasema rushwa ni tatizo kwa wote

Josephat Nyiro Charo3 Desemba 2014

Katika ripoti yake ya leo (03.12.2014) shirika hilo lilisema rushwa inaonekana kukithiri Uturuki na China na limetaka kuwepo ushirikiano wa karibu wa kimataifa kuangamiza kabisa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

https://p.dw.com/p/1Dyao
Symbolbild Geldwäsche Korruption Bestechung
Picha: Fotolia/flyinger

Katika ripoti yake shirika la Transparency International hilo lenye makao yake Berlin Ujerumani lilisema rushwa ni tatizo kwa uchumi na kuna umuhimu wa taasisi kubwa za fedha katika Umoja wa Ulaya na Marekani kufanya kazi pamoja na nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kuwakomesha mafisadi wasikwepe mkono wa sheria.

Katika faharasa ya 20 inayoonyesha viwango vya rushwa katika mataifa 175, China imepata alama 36 kati ya 100, Uturuki imepata 45 na Angola 19, zikiwa nchi ambazo zimeanguka kwa alama kati ya 4 na 5, licha ya uchumi wao kukua kwa wastani wa asilimia 4 katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Transparency International hutoa alama 100 kwa nchi ambayo haina visa vya rushwa na sufuri kwa nchi ambayo rushwa imeshamiri.

Kwa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki, Rwanda imefanya vyema katika kupambana na rushwa ikishikilia nafasi ya 55, ikifuatiwa na Tanzania katika nafasi ya 119, na Uganda ni ya tatu katika nafasi ya 142. Kenya ni ya nne katika nafasi ya 145 na Burundi inashika mkia katika jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa katika nafasi ya 159.

Zaidi ya theluthi mbili kati ya nchi 175 katika faharasa hiyo zimepata pointi chini ya 50 huku Somalia, Korea Kaskazini, Sudan, Afghansitan na Sudan Kusini kwa mara nyingine tena zikishika nafasi za chini.

Mkurugenzi wa Transparency International katika mataifa yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara, Chantal Uwimana, alisema, "Vipindi vya mizozo huchochea rushwa, kuyumba kwa hali ya kisiasa na kukosekana uthabiti kwa sababu mifumo hudhoofika au wale wanaotakiwa kuisimamia mifumo hii wanapoteza muelekeo.Si jambo la kushangaza kwamba Sudan Kusini na Somalia ambazo zimekabiliwa na vita kwa muda mrefu zinaonekana kuwa na vitendo vya rushwa iliyokithiri."

Denmark ni mfano wa kuigwa

Nchi iliyofanya vizuri kabisa na kushika nafasfi ya kwanza ni Denmark ikijipatia pointi 92, ikifuatiwa na New Zealand, Finland, Sweden na Norway, zote kwa mara nyingine tena zikiwa katika tabaka la nchi tano za kwanza aktika faharasa ya rushwa.

Infografik Korruptionsindex 2014 Englisch
Faharasa kuhusu rushwa ya mwaka 2014

Ukraine ilipata pointi 26 na kubakia kuwa nchi inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha rushwa barani Ulaya. Italia,Ugiriki na Romania kwa pamoja zimafanya vibaya miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zikiwa na pointi 43.

Mwenyekiti wa Transparency International, José Ugaz alisema maafisa mafisadi huficha mali walizozipata kwa njia isiyo halali na kuzificha katika maeneo salama kupitia kampuni. Ugaz aidha amesema ufisadi mkubwa katika nchi zenye uchumi mkubwa haukandamizi tu haki za binadamu kwa watu masikini, bali pia husababisha matatizo ya utawala na uthabiti.

Ripoti hiyo ilizitaka nchi zinazoshika mkia katika orodha iliyochapishwa zichukue hatua madhubuti za makusudi kupambana na rushwa kwa masilahi ya umma. Ugaz aliyataka mataifa yanayoshika nafasi za juu katika faharasa hiyo yasieneze vitendo vya ufisadi katika nchi ambazo hazijaendelea.

Shirika la Transparency International liliuhimiza Umoja wa Ulaya, Marekani na kundi la G20 la mataifa yaliyostawi na yanayoinukia kiuchumi, kuiga mfano wa Denmark na kuanzisha daftari la umma linalojumuisha tarifa muhimu za wamiliki kwa kampuni zote zilizoshirikishwa.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE

Mhariri:Saumu Yusuf