1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aanza vyema safari yake ya kuwania urais Marekani

Mohammed Khelef
16 Januari 2024

Donald Trump ameanza vyema safari yake ya kurejea katika Ikulu ya Marekani, baada ya kushinda uchaguzi wa kwaza wa mchujo katika jimbo la Iowa kuwania uteuzi wa chama cha Republican kugombea urais mwezi Novemba.

https://p.dw.com/p/4bK35
USA Iowa Caucus | Des Moines | Trump
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump akisherehekea ushindi wa mchunjo katika jimbo la lowa, unaoweza kummpa nafasi ya kuwania urais katika uchaguzi wa Novemba kupitia chama cha Republican.Picha: UPI Photo/IMAGO

Safari ya gavana huyo wa Florida kuelekea Ikulu ya White House iko mashakani kisiasa na kifedha, baada ya kufanya vibaya kwenye kura ya kwanza ya mchujo katika jimbo la Iowa juzi Jumatatu.

Licha ya kuwekeza sana muda na rasilimali kwenye jimbo hilo, la kwanza kuanza uchaguzi wa mchujo wa vyama nchini Marekani, DeSantis alimalizikia akiwa ameachwa nyuma kwa takribani asilimia 30 na rais wa zamani, Donald Trump, na akiwa amempita kidogo sana mfuatizi wake,  balozi wa zamani wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Nikki Haley. DeSantis, alipata asilimia 21, Haley akiwa na asilimia 19, lakini Trump aliwapiku akiwa na asilimia 51.

Mwaka mmoja uliopita, DeSantis alionekana kama mpinzani wa kwelikweli dhidi ya uwezo wa Trump kukitia mfukoni chama kizima cha Republican. Lakini kwa kipindi sasa, maoni ya wapigakura kwake yamekuwa yakishuka kwa kasi na amekuwa na nafasi mbaya zaidi kwenye majimbo yanayoitwa muhimu sana kwenye uchaguzi wa Marekani, hasa baada ya kuamua kuwekeza muda na rasilimali nyingi jimboni Iowa. Hilo linamfanya sasa kuwa kwenye nafasi ya kutoweza kurejea katika nafasi yake ya awali.

Biden aonya juu ya urais wa Donald Trump wakati wa kukumbuka uvamizi wa jengo la Bunge, Januari 6, 2021

Hivi sasa tayari yuko jimboni New Hampshire kuendeleza kampeni yake, lakini hili ni jimbo ambalo tangu hapo aliwekeza muda mchache sana na ambalo tayari kura za maoni zinamuweka nafasi ya tatu, nyuma ya Haley na Trump. Jimbo hilo ndilo linalofuatia kwenye upigaji wa kura za mchujo za Republican, Jumanne wiki ijayo. DeSantis pia anashika mkia kwenye jimbo la South Carolina, ambalo linapiga kura mwishoni mwa mwezi Februari.

Trump apewa nafasi kubwa ya kuwa mgombea wa Republican katika uchaguzi ujao

Marekani | Iowa Caucus | Donald Trump
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump Picha: Evelyn Hockenstein/REUTERS

Kirk Jowers, ambaye amekuwa kwenye kampeni za marais watano wa Republican na ambaye ni mshauri wa wafadhili wa DeSantis, anaona kwamba kwa mgombea wake huyo mambo yamekwisha.

Kirk anasema na hapa namnukuu: "Matokeo ya Iowa yanathibitisha bila tone la shaka kwamba Trump ndiye atakayekuwa mgombea na hakuna yeyote awezaye kuzuwia hilo, isipokuwa Mungu au mahakama. Na vile vile, hakuna kiwango cha ufadhili ama kazi ya kujitolea itakayoweza kumuweka DeSantis au Halley mbele ya Trump." Mwisho wa kumnukuu.

Chanzo kimoja kwenye timu ya DeSantis kimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba gavana huyo anakabiliwa na matatizo ya kugharamikia kampeni yake, ingawa hakusema moja kwa moja kwamba kuna hatari ya kumalizikiwa na fedha muda mfupi ujao.

Mahakama Colorado imemzuia Donald Trump kuwania urais jimboni humo

Baadhi ya washirika wa gavana huyo wanamtia moyo kwamba asonge mbele, na wachambuzi huru wanasema japokuwa usiku wa Jumatatu ulikuwa mbaya kwa DeSantis, lakini haukuwa mbaya zaidi ya ulivyotarajiwa, kwani kura za maoni zilikuwa zimeonesha akishika nafasi ya tatu. Roy Bailey, mmoja wa wachangishaji fedha wakubwa wa DeSantis, anasema wana fedha za kutosha kuwafikisha hadi kile kinachoitwa Jumanne Kuu, ambapo kura kadhaa za mchujo zinapigwa kwa siku moja mwanzoni mwa mwezi Machi.

Lakini, hata awe na fedha za kutosha, DeSantis hana vibwagizo vya kampeni alivyonavyo Trump, ambaye uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa zaidi ya nusu ya wapigakura wa Republican wanayaamini madai yake kwamba aliibiwa ushindi wake kwenye uchaguzi wa mwaka 2020. Zaidi ya asilimia 60 wanasema kuwa bado Trump anafaa kuwa rais hata kama atatiwa hatiani kwa uhalifu anaoshitakiwa nao katika jumla ya mashitaka 91 yanayomkabili mahakamani hivi sasa.

reuters