1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asisitiza kuhusu kuyaondoa majeshi yake Syria

Grace Kabogo
4 Aprili 2018

Rais wa Marekani, Donald Trump amesisitiza juu ya azma yake ya kuyaondoa majeshi ya Marekani nchini Syria na kusema kwamba atatoa uamuzi wake hivi karibuni kuhusu kupunguza msaada nchini humo.

https://p.dw.com/p/2vS6q
USA Washington - Donald Trump verhängt Strafzölle gegen China
Picha: Reuters/J. Ernst

Trump ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi habari pamoja na viongozi wa mataifa ya Baltic. Amesema lengo hasa la majeshi ya Marekani lilikuwa kuwaondoa wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS na kwamba wanakaribia kuikamilisha kazi hiyo.

''Nataka kuondoka. Nataka kuwaleta wanajeshi wetu nyumbani. Nataka kuanza kulijenga upya taifa letu. Tumefanikiwa sana dhidi ya IS. Tutashinda kijeshi dhidi ya mtu yeyote. Lakini umefika wakati wa kurudi nyumbani na tunalifikiria jambo hilo kwa umakani,'' alisema Trump.

Trump amesema Marekani imetumia Dola trilioni 7 katika Mashariki ya Kati kwa miaka 17 iliyopita na haijanufaika chochote zaidi ya vifo na uharibifu na hilo ni jambo la kutisha. Wiki iliyopita Trump alisema Marekani itaondoka Syria hivi karibuni.

Syrian Ost-Ghouta Arbin Ruinen
Mji wa Ghouta Mashariki, Syria Picha: picture-alliance/AA/Al-Din Samout

Hata hivyo, uamuzi wa Trump unakinzana na mtazamo wa washauri wake wa ngazi ya juu. Mjumbe maalum wa Marekani anayeratibu muungano wa kimataifa unaopambana na IS, Brett McGurk amesema jana kuwa wanajeshi wa Marekani wako Syria kupambana na IS na kwamba kazi yao bado haijakamilika na wataikamilisha.

Maafisa waliouandaa mkutano huo, wamesema timu yote ya usalama ya Trump, akiwemo mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA Mike Pompeo, ambaye ameteuliwa kuwa waziri mpya wa mambo ya nje, wamepinga kuondolewa haraka wanajeshi hao.

Saudia yatakiwa kuchangia Dola bilioni 4

Katika wiki za hivi karibuni, Trump aliitaka Saudi Arabia kuchangia Dola bilioni 4 kwa ajili ya kuijenga upya Syria, kama sehemu ya juhudi za kiongozi huyo kuzitaka nchi nyingine zichangie katika kutuliza hali ya Syria na Marekani inasubiri jibu kutoka kwa Saudia.

Afisa wa ngazi ya juu wa Wakurdi wa Syria, Ilham Ahmed, amesema matamshi ya kuyaondoa majeshi ya Marekani nchini Syria yametolewa kipindi kibaya, wakati ambapo wapiganaji wa IS wameibuka tena mashariki mwa Syria na kuwepo kwa vitisho kutoka kwa Uturuki.

Hayo yanajiri wakati ambapo viongozi wa Iran, Urusi na Uturuki wanakutana leo mjini Ankara kwa lengo la kuharakisha mchakato wa amani ya Syria pamoja na kuimarisha ushawishi wao nchini humo.

Russland | Präsidenten Erdogan, Putin und Rouhani
Rais Rouhani akiwa na Rais Putin na Rais ErdoganPicha: picture-alliance/AP Images/K. Ozer

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan atakuwa mwenyeji wa viongozi wenzake wa Urusi, Vladmir Putin na Iran, Hassan Rouhani katika mkutano ambao huenda ukazaa matunda ya kupatikana kwa amani ya Syria. Mkutano huo wa pande tatu ni wa pili kufanyika kati ya viongozi hao, ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika Sochi, Urusi mwezi Novemba.

Nchi hizo tatu zinaunga mkono mazungumzo ya amani yanayofanyika kwenye mji mkuu wa Kazakhstan, Astana ambayo wamesema ni sambamba na yale yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yanayofanyika mjini Geneva, Uswisi.

Wakati Urusi na Iran zinaiunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad kisiasa na kijeshi, Uturuki kwa upande wake imerudia wito wake wa kutaka kiongozi huyo aondolewe madarakani na inawaunga mkono wapiganaji wa makundi ya waasi nchini Syria.

Mhariri: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga