1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuondoka ikulu baada ya Biden kuthibitishwa mshindi

Lilian Mtono
27 Novemba 2020

Rais Donald Trump wa Marekani amesema kwa mara ya kwanza Alhamisi hii kwamba ataondoka ikulu ya White House iwapo rais mteule Joe Biden atathibitishwa rasmi kuwa mshindi wa uchaguzi wa Marekani.

https://p.dw.com/p/3ltOv
USA | PK | Präsident Donald Trump
Picha: Kevin Dietsch//UPI Photo/imago images

Hata hivyo Trump bado anaendeleza madai yake kwamba uchaguzi huo kuvurugwa. 

Trump alifanya majaribio kadhaa ambayo hayakutarajiwa ya kuyakataa matokeo ya uchaguzi kwa kukataa kukubali kushindwa, huku akiibua nadharia kadha wa kadha kuhusu kuibiwa kura na hata kufungua madai yasiyo na uthibitisho mahakamani, ambayo hata hivyo yalitupiliwa mbali na mahakama za Marekani.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari tangu uchaguzi wa Novemba 3, rais Trump alionekana kukaribia kukubali kwamba atahudumu kwa muhula mmoja kabla ya Biden kuapishwa Januari 20 mwakani.

Na baada ya kuulizwa iwapo ataondoka White House, kama jopo la wajumbe maalumu wa uchaguzi la Electoral College litauthibitisha ushindi wa Biden, Trump alikubali kwamba ataondoka na kuongeza kuwa hata waandishi hao wa habari wanajua kwamba ataondoka.

"Ni dhahiri nitaondoka. Lakini ninadhani kwamba kutakuwepo na mengi yatakayotokea kati ya sasa na hiyo Januari 20. Mambo mengi. Udanganyifu mkubwa umegundulika", alisema Trump.

USA Washington | Donald Trump begnaded zwei Truthähne zu Thanksgiving
Rais Donald Trump alikuwa akizungumza kwenye sikukuu za Thanks Giving katika ikulu ya White HousePicha: Hannah McKay/REUTERS

Wajumbe wa Electoral College ambao huamua kuhusu mshindi anayeingia ikulu ya White House watakutana Disemba 14 kuthibitisha ushindi wa Joe Biden, ambaye amejinyakulia kura 306 za wajumbe hao dhidi ya mpinzani wake Trump aliyepata kura 232.

Trump alirudia matamshi yake kwamba uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu mkubwa bila ya kutoa uthibitisho wowote wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika ikulu ya White House baada ya kuzungumza na wanajeshi kupitia video kwenye maadhimisho ya sikukuu ya Thanks Giving. Amesema pamoja na matokeo ya sasa, lakini huenda sikukuu hii haitakuwa ya mwisho kwake kusherehekea akiwa ikulu ya White House.

Aidha Trump ameifananisha miundombinu ya uchaguzi ya Marekani na ya mataifa ya ulimwengu wa tatu na mapema jana aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba uchaguzi ulivurugwa kwa asilimia 100.

USA Wilmington, Delaware | Joe Biden, Vorstellung Team | Joe Biden
Rais mteule Joe Biden anakabiliwa na changamoto kubwa ya vita dhidi ya janga la corona nchini Marekani.Picha: Mark Makela/Getty Images

Na kuelekea kwa wajumbe wa Electoral College, Trump ameweka wazi kwamba huenda kamwe asitamke rasmi kushindwa, hata kama ataondoka ikulu. Amenukuliwa akisema "itakuwa vigumu mno kukubali kushindwa, kwa sababu kila mtu anajua kulikuwa na uvurugwaji mkubwa na kusisitiza kwamba muda hauko upande wao.

Hatua ya Trump ya kukataa kukubali kushindwa inaongeza idadi ya tamaduni za taifa hilo alizozivuruga katika kipindi chake cha miaka minne. Wafuasi wake wanadhani kwamba tayari ameanza kuangazia kugombea uchaguzi wa mwaka 2024. Hata hivyo, hakutaka kulizungumzia hilo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari.

Na alipoulizwa kuhusu iwapo atahudhuria shughuli za kuapishwa Biden, alisema analijua jibu, lakini asingependa kuweka wazi kwa sasa.

Kuhusiana na chanjo ya virusi vya corona, Trump aliwaonya waandishi kutompa sifa Biden juu ya kupatikana kwa chanjo hiyo, akisema hizo ni juhudi zake na ni shinikizo lake kubwa ambalo halijawahi kutokea huko nyuma ambalo limepelekea kupatikana kwake.

Rais mteule Joe Biden amekwishasema kwamba Wamarekani hawatavumilia majaribio ya kuyageuza matokeo ya uchaguzi, huku akiwatolea mwito wa kuungana kupambana na janga linalozidi kushika kasi nchini humo la COVID-19. Zaidi ya watu 260,000 wamekufa kutokana na virusi vya corona huku idadi ya vifo vya kila siku ikiongezeka hadi 2,000 katika siku za karibuni.

Soma Zaidi: Biden: Watu zaidi huenda wakafa Trump asipotoa ushirikiano