1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump vs dunia:G-20 wagawanyika kuhusu biashara, tabianchi

Iddi Ssessanga
1 Desemba 2018

Migawanyiko miogoni mwa mataifa yanayoongoza kwa uchumi duniani imejitokeza tangu viongozi wake walipokusanyika Ijumaa nchini Argentina katika mkutano wao wa kiele wa mwaka.

https://p.dw.com/p/39FVo
Argentinien G20 Gipfel - Gruppenfoto
Picha: picture-alliance/AA/Turkish Presidency/M. Cetinmuhurdar

Wajumbe wa majadiliano wa Marekani walizuwia maendeleo katika mkutano wa kilele wa G20 kuhusu kusimamia uhamiaji, kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi, na kusawazisha uendeshaji wa biashara ya dunia, kwa mujibu wa maafisa wa Ulaya wanaoshiriki mazungumzo hayo.

Wasiwasi wa usalama ulipewa uzito pia kwenye mkutano huo wa siku mbili mjini Buenos Aires. Waziri wa usalama wa Argentina alisema mabomu manane ya petroli yaligunduliwa katika eneo la mji mkuu lililoko km kadhaa kutoka eneo la mkutano huo, ambako maandamano yaliyofanyika mchana yalihudhuriwa na maelfu ya watu waliobeba mabango yenye ujumbe kama "Ondoka G-20" na "Ondoka Trump."

Mantiki ya kundi la G-20 - lililoundwa kufuatia mgogoro wa kifedha wa dunia muongo mmoja uliopita - ni kutafuta njia za kutatua matatizo ya dunia kwa pamoja, lakini wanadiplomasia mjini Buenos Aires walipambana kutafuta masuala ya kutosha ambayo viongozi wote wanakubaliana juu yake.

Trump alitaka kuutumia mkutano huo kufanya makubaliano yake ya kibiashara, na aliwakasirisha wenyeji wa mkutano huo Argentina kwa kufasili vibaya msimamo wao kuhusu matendo ya kibishara ya China.

Argentinien G20 Gipfel - Putin und bin Salman
Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman akifurahia jambo na rais wa Urusi Vladmir Putin wakati wa mkutano wa kilele wa G-20 mjini Buenos Aires, Argentina, Novemba 30, 2018.Picha: picture alliance/AP Photo/N. Pisarenko

Putin, Bin Salman waliwazana mbele ya ukosoaji

Wakati huo huo, viongozi wawili wanakabiliwa na ukosoaji kutoka mataifa ya magharibi hivi karibuni - Rais wa Urusi Vladmin Putin na Mrithi wa kiti cha ufalme Mwanamfalme Mohammed bin Salman - walionekana kuliwazana, kwa kupeana mikono wakati wakikaa chini kwa ajili ya mazungumzo.

Rais wa Argentina Mauricio Macri alifungua mkutano huo kwa kukiri migawanyiko ndani ya kundi hilo la G-20 huku akiwasihi viongozi wa dunia kuzingatia haja ya uharaka na kuchukuwa hatua kwa msingi wa maslahi ya pamoja.

Wanadiplomasia kutoa mataifa ya G-20 walikuwa wanabishana vikali kuhusiana na taarifa ya mwisho ya mkutano huo, ambapo migawanyiko mikubwa kuhusu lugha gani ya kutumiwa kuhusu makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi na shirika biashara duniani, WTO. Maafisa wawili wa Ulaya wanaoshirikia majadiliano walisema Marekani ilikuwa inazuwia maendeleo kuhusu masuala hayo mawili.

Marekani kuwekwa kando

G20 Argentinien 2018 Donald Trump und Mauricio Macri
Rais wa Marekani Donald Trump (kushoto) akipeana mkono na Rais wa Argentina Mauricio Macri kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa G-20, Novemba 30, 2018.Picha: picture-alliance/dpa/P. M. Monsivais

Hivyo jibu lisilofuata desturi likaibuka: Afisa kutoka ofisi ya rais wa Ufaransa alisema taarifa hiyo huenda ikawa na lugha inayoitenga Marekani. Kwa mfano, rasimu inasema washiriki 19 wanakubaliana kuhusu umuhimu wa kuyaendeleza makubaliano ya Paris, lakini Marekani haikubaliani.

Alipoulizwa kuhusu wasiwasi wa mataifa ya Ulaya, afisa wa Marekani alisema hatua zilikuwa zinapigwa kuhusu taarifa ya pamoja na kwamba Ikulu ya White House ilikuwa na matumaini kuhusu waraka huo kwa ujumla. Baadae afisa wa Argentina anaeongoza mazungumzo ya G-20 kuhusu masuala ya kifedha Laura Jaitman, alisema Trump alikuwa anashughulika sana na amejiwekea sharti katika majadiliano hayo na kusema hatua zilipigwa katika mazungumzo ya Ijumaa kuhusu fedha za biashara.

"Kuna ujumbe chanya wa namna biashara imekuwa kichocheo cha ukuaji kwa miongo ijayo na namna itaendelea huko mbeleni kutoa manufaa kwa raia wote," alisema Jaitman. Waziri wa mambo ya nje wa Argentina Jorge Faurie alisema mazungumzo ya biashara yalikuwa yanasonga mbele na mataifa yalikuwa yanaendelea kufanyia kazi tangazo kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Licha ya Trump kupuuza wasiwasi kuhusu kuongozeka kwa joto la dunia, China, Ufaransa na Umoja wa Mataifa walikuja pamoja siku ya Ijumaa kuunga mkono mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Tangazo lao lilinuwia kuwahamasisha wanachama wengine wa G-20 kuchukuwa hatua sawa, na kutoa msukumo kwa mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu mbadiliko ya tabianchi.

G20-Gipfel in Argentinien - Protestmarsch Soldaten
Askari wa usalama wakisimama mbele ya kundi la waandamanaji wanaopinga mkutano wa G-20 mjini Buenos Aires, Argentina, Novemba 30, 2018.Picha: picture-alliance/dpa/C. Santisteban

Mada kuu zawekwa pembeni

Kwa ujumla, mkutano wa G-20 unanuwiwa kujikita kwenye masuala kwama ajira, miundombinu, maendeleo, utulivu wa kifedha na biashara ya kimataifa. Lakini wakati mkutano huo ukianza, mada hizo zilionekana kama mawazo ya baadae, zikifunikwa na masuala tete kuanzia mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na China hadi mgogoro kati ya Urusi na Ukraine.

Karibu maafisa 22,000 wa polisi na vikosi vingine vya usalama wanalinda viongozi wakati wa mkutano huo. Argentina ndiyo nchi ya kwanza ya Amerika Kusini kuwa mwenyeji wa mkutano wa G-20, na maafisa wamefanya juhudi kuhakikisha kwamba fujo zinadhibitiwa kuliko ilivyokuwa katika mkutano wa mwaka uliiopita mjini Hamburg, Ujerumani, ambako makabiliano yalizuka katika kati ya polisi na waandamanaji.

Maafisa wa serikali ya Argetina wamesema hawatovumilia vurugu au kuruhusu mkutano huo kuvurugwa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Daniel Gakuba