1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai afuta mpango wa kurudi Zimbabwe kutokana na njama ya kutaka kumuuwa.

Mohamed Dahman17 Mei 2008

Hofu za njama ya mauaji dhidi ya kiongozi wa upinzani Zimbabwe imechelewesha kurudi kwake nchini humo kulikokuwa kukisubiriwa kabla ya marudio ya uchaguzi dhidi ya Rais Robert Mugabe hapo tarehe 27 mwezi wa Juni.

https://p.dw.com/p/E1jE
Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai.Picha: AP

Baada ya kuwepo nje kwa zaidi ya mwezi mmoja Morgan Tsvangirai alikuwa akitarajiwa kurudi nyumbani leo hii lakini amebadili mipango dakika ya mwisho baada ya kudokezwa juu ya jaribio la kutaka kumuuwa.

Msemaji wa kiongozi huyo George Sibotshiwe amesema wamepokea habari kutoka duru za kuaminika asubuhi hii ya kuwepo kwa mpango wa kumuuwa Tsvangirai. Msemaji huyo anasema kwa hivi sasa hawawezi kusema iwapo mpango huo umeungwa mkono na serikali na habari hizo tayari wamezifikisha kwa wakuu wengine wa nchi na kwamba ni jambo la uhakika kusema kuna ni tishio zito dhidi ya maisha yake na wanaamini kutokana na ushauri wa wanausalama wao isingelikuwa jambo la busara kwa Tsvangirai kwenda Zimbabwe leo hii.

Tsvangirai ambaye mwishoni mwa juma lililopita alisema angelirudi Zimbabwe hivi karibuni alitowa madai kadhaa ya kutaka kuhakikishwa maradio ya uchaguzi huo yanakuwa huru na wa haki ikiwa ni pamoja na kupelekwa nchini humo kwa wanajeshi wa kulinda amani wa kigeni na waangalizi wa uchaguzi.