1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Sudan

Oumilkher Hamidou6 Aprili 2010

Maoni ya wamarekani kuhusu uchaguzi mkuu nchini Sudan

https://p.dw.com/p/MoEv
Rais Omar Al Bashir wa SudanPicha: AP

Matamshi ya mjumbe wa Marekani huko Sudan kuwa uchaguzi utakaofanywa utakuwa "huru na wa haki kama iwezekanavyo" yamekosolewa kote Marekani na Sudan, kuhusu sera ya Washingaton kuelekea nchi hiyo katika bara la Afrika.

Matamshi ya mjumbe wa Marekani Scott Gration nchini Sudan yametolewa huku vyama vingi vikuu vya upinzani nchini humo vikisusia uchaguzi wa rais. Juma lililopita,Yassir Arman, mpinzani mkuu wa Rais wa Sudan Omar al-Bashir, alitangaza kuwa hatogombea uchaguzi huo kwa sababu ya masuala ya usalama, mgogoro wa Darfur unaoendelea na kwa sababu ya mambo yasio ya kawaida katika maandalizi ya uchaguzi.

Arman aliungwa mkono na chama cha Sudan ya Kusini cha SPLM, kilichopigana vita vya wenyewe kwa wenyewe na serikali ya Sudan kwa miaka 22. Vita hivyo vilimalizika mwaka 2005 kufuatia makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya chama cha SPLM na chama tawala NCP cha Rais al-Bashir.

Lakini licha ya vyama vingi vya upinzani kususia uchaguzi ujao wa rais, mjumbe wa Marekani nchini Sudan,Scott Gration ametetea hadharani chaguzi zitakazofanywa tarehe 11 hadi 13 mwezi huu wa Aprili. Amesma:

"Watu hawa wamejitahidi sana kuhakikisha kuwa wananchi wa Sudan wataweza kufika kwenye vituo vya kupigia kura na taratibu za chaguzi zitahakikisha kuna hali ya uwazi."

Hizo zitakuwa chaguzi za kwanza kufanywa nchini Sudan tangu zaidi ya miaka 20 iliyopita. Wapiga kura watachagua rais,bunge na serikali za mitaa. Chama cha SPLM kimesusia uchaguzi wa rais, lakini kimeamua kugombea chaguzi za bunge na serikali za mitaa. Lakini baada ya Arman kujitoa katika kinyanganyiro cha uchaguzi wa rais, rais wa sasa al-Bashir hakabiliwi tena na changamoto kali. Katika mwaka 2008, Rais Bashir binafsi alishtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu nchini Uholanzi ICC kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan.

Wasiwasi kuhusu mambo yasio ya kawaida katika utaratiibu wa uchaguzi pamoja na mashtaka ya ICC yamewafanya baadhi ya walimwengu kuuliza kwanini Marekani inaunga mkono kile kilichoelezwa kama " utaratibu wa uchaguzi ulio na hila." John Prendergast, aliekuwa mkurugenzi wa masuala ya bara la Afrika katika Baraza la Usalama wa Taifa katika serikali ya rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, ni miongoni mwa wale walioshangazwa na matamshi ya Gration. Yeye amesema, matamshi ya Gration kuhusu Sudan hayaaminiki tangu muda kadhaa. Prendergast akiikosoa sera ya Marekani kuelekea Sudan,amesema sera hiyo imejengeka kwa msingi wa kile ambacho wangependelea.

Mwandishi:MartinPrema/IPS

Mhariri: M.Abdul-Rahman