1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Uingereza na kura ya maoni ya Uturuki Magazetini

Oumilkheir Hamidou
19 Aprili 2017

Mada mbili kuu magazetini : Uamuzi wa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wa kuitisha uchaguzi kabla ya wakati, na suali kwanini Wajerumani wenye asili ya Uturuki wamepiga kura kwa wingi kuunga mkono mageuzi ya katiba

https://p.dw.com/p/2bTqr
England Premierminister Theresa May
Picha: Reuters/S. Wemuth

Tunaanzia Uingereza ambako wakaazi wa nchi hiyo ya kifalme sawa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanaendelea kujiuliza kwanini waziri mkuu Theresa May amebadilisha msimamo wake na kuamua kuitisha uchaguzi kabla ya wakati. Gazeti la "Rhein-Necker" la mjini Heidelberg linaandika: "Ni sababu za kibinafsi na kujipendelea bila ya shaka"-wakosoaji wanahofia aina ya mapinduzi kutoka juu. Umashuhuri wake umeongezeka kwa nguvu kuliko wakati wowote ule mwengine. Huu kwa hivyo ndio wakati muwafak kuudhoofisha upande wa upinzani wa Labour, kuzisuta hoja za wale wanaosema anatawala bila ya kuchaguliwa na pia kuimarisha msimamo wake katika majadiliano ya Brexit dhidi ya viongozi wa umoja wa ulaya mjini Brussels .

Hoja za waziri mkuu May hazina msingi

Gazeti la mjini Cologne, Kölner Stadt Anzeiger linazitaja hoja zilizotolewa na waziri mkuu wa Uingereza kuitisha uchaguzi wa bunge kabla ya wakati kuwa "uwongo mtupu". Gazeti linaendelea kuandika: "Theresa May anasema anaitisha uchaguzi wa kabla ya wakati ili kupata uongozi imara. Katika wakati ambapo nchi imeungana upya baada ya kura ya Brexit, kuna mfarakano katika bunge anahoji waziri mkuu Theresa May. Hali kama hiyo haifai katika kuendeleza majadiliano ya Brexit. Hoja zote hizo ni za uwongo linasema gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linalohisi wahafidhina wana sababu moja tu: chama chao kinaongoza katika tafiti za maoni ya wapiga kura kwa asili mia 20 mbele ya upande wa upinzani wa Labour. Wakifanikiwa kunusuru angalao nusu ya kiwango hicho, basi Theresa May ataweza kutegemea wingi mkubwa kabisa kuweza kutawala bila ya shida. Hoja zake kuhusu masilahi ya taifa ni za hadaa."

Majadiliano kunusuru mshikamano

Yalikuwa maoni ya gazeti la mjini Cologne kuhusu uamuzi wa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wa kuitisha uchaguzi mkuu kabla ya wakati. Mada ya pili iliyohanikiza magazetini nchini Ujerumani inahusu matokeo ya kura ya "Ndio" inayompatia madaraka makubwa zaidi rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Takriban wahariri wote wa magazeti wanajiuliza kwanini Wajerumani wenye asili ya Uturuki na wanaoishi humu nchini wameamua kuiunga mkono kura hiyo ya maoni? Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linajaribu kulijibu suali hilo: "Kwamba takriban thuluthi mbili ya wajerumani wenye asili ya Uturuki wameunga mkono katiba inayofanana na ile ya utawala wa kiimla, suala hilo linahitaji kweli ufafanuzi. Na hapa pia vyombo vya habari vimechangia. Wajerumani wengi wenye asili ya Uturuki wanajipasha habari kupitia vyombo vya habari vya Uturuki ambavyo takriban vyote vinadhibitiwa na Erdogan. Katika vyombo hivyo vya habari na pia katika misikiti inayaosimamiwa na serikali ya mjini Ankara, wanaambiwa eti Ulaya inataka kuidhoofisha Uturuki na kwamba eti vyombo vya habari vya Ujerumani vinazua . Mdahalo unahitajika, katika kila mji. Sio kwa kutupiana lawama bali kwa mtazamo sawia. Mwenye kutaka watu waishi pamoja hawezi kulikwepa hilo-tena kutoka pande zote mbili.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Josephat Charo