1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa vyombo vya habari Afrika mashakani: Ripoti

12 Februari 2014

Ripoti ya Shirika la maripota wasio na mpaka mwaka 2014 linasema migogoro barani Afrika imezidisha hatari kwa uhuru wa kujieleza, likisema hali hiyo imedhihirika bayana nchini Mali na katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/1B7Cz
Waandishi wa habari nchini Burundi wakiandamana kutetea uhuru wao
Waandishi wa habari nchini Burundi wakiandamana kutetea uhuru waoPicha: Esdras Ndikumana/AFP/Getty Images

Ripoti ya mwaka 2014 kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, hususan barani Afrika, inajikita juu ya namna migogoro mipya barani humo inavyoambatana na changamoto za kipekee juu ya uhuru wa habari. Kwa mfano, baada ya wanajeshi kuiangusha serikali ya Mali mwaka 2012, hatua ya kwanza waliyoichukua ilikuwa kukiteka kituo cha taifa cha Televisheni na radio.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, makundi yenye mielekeo ya kisiasa hutumia silaha za kivita kujinufaisha kiuchumi, na hujitahidi kudhibiti vyombo vya habari kwa maslahi yao. Mfano unaotolewa ni wa kundi la waasi wa M23, ambalo ripoti hiyo inasema liliyakagua magazeti kabla ya kuruhusu yasambazwe katika maeneo lililokuwa likiyashikilia, na liliwatisha mameneja wa vituo vya radio ambavyo vilitangaza habari ambazo zililikosoa kundi hilo.

Mizozo mipya ya kisiasa

Katika Jamhuri ya Afrika Kati, ambako hakukuwa na mshindi wa dhahiri kati ya muungano wa makundi ya waasi wa Seleka na wanajeshi waliomtii rais aliyepinduliwa na Seleka, Francois Bozize, maafisa wakuu wa polisi waliwahoji wenyewe na kuwatisha waandishi ambao walidiriki kuzungumzia uwezekano wa kulifanyia marekebisho baraza la mawaziri.

Mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati umezidisha ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari
Mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati umezidisha ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habariPicha: picture alliance/AP Photo

Ripoti hii inaeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari uliendelea kudidimia katika eneo zima la Afrika ya Kati, kuanzia nchi za mwambao wa Bahari ya Atlantiki hadi kanda za maziwa makuu. Inasema hali ni mbaya zaidi katika Guinea ya Ikweta, nchi pekee inayozungumza kihispania katika eneo hilo. Ripoti inasema hakuna mwandishi hata mmoja aliyeripotiwa kunyanyaswa, kwa sababu wote wamezibwa mdomo, na kwa hivyo ama hujiwekea mipaka wenyewe, au huikimbia nchi.

Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mgogoro wa umwagaji damu umeyafanya magazeti yaegemee upande mmoja na kuchochea vurugu zaidi kuliko kuupasha umma habari za kuaminika. Nchini Chad, ambako uongozi ni wa kiimla, waandishi 23 wa habari walikamatwa mwaka 2013, na ingawa waliachiwa baadaye, lakini hawakuweza tena kutangaza habari kwa njia huru. na huko Angola, mwandishi wa habari Rafael Marques de Morais amekamatwa na kuhojiwa mara kadhaa, baada ya kuchapisha kitabu kinachochambua maovu yanayofanywa katika sekta ya almasi nchini humo.

Burundi imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya chini juu kutunga sheria zinazokandamiza zaidi uhuru wa vyombo vya habari.

Kundi la Boko Haram huuwa waandishi na kuharibu magazeti
Kundi la Boko Haram huuwa waandishi na kuharibu magazetiPicha: AP

Mwiko kuitaja Boko Haram

Kwingineko barani Afrika, kundi la Boko Haram nchini Nigeria ambalo linashukiwa kuwa na mafungamano na mtandao wa al-Qaida, linatajwa katika ripoti hiyo kwamba liliwauwa waandishi wawili walioandika taarifa ambazo lilizichukuliwa kuwa si sahihi, na limeyaharibu magazeti kwa kuyapiga mabomu. Kutangaza chochote juu ya kundi hilo ni mwiko.

Katika eneo la pembe ya Afrika, Eritrea imeelezwa kuwa gereza kubwa kwa waandishi wa habari kwa kuwa na waandishi 28 wanaosota jela, nako nchini Somalia, waandishi wanaojaribu kutoa taarifa zisizoegemea upande wowote wamejikuta wakiwindwa na pande zote, yaani serikali na waasi wa al-Shabaab. Mwaka 2013, waandishi saba waliuawa nchini humo.

Hata hivyo ripoti hiyo inafurahia kuibuka kwa teknolojia inayowawezesha watu kupata habari kupitia njia nyingi zaidi, tofauti na siku za nyuma ambako radio na magazeti ilikuwa njia pekee y kupata habari. Daniel Gakuba anakupasha zaidi katika taarifa ifuatayo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/http://rsf.org/index2014/en-africa.php

Mhariri:Hamidou Oummilkheir