1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wazidi kuporomoka Ujerumani na Uturuki

Sekione Kitojo
11 Septemba 2017

Wajerumani wawili wengine wanaaminika wamekamatwa nchini Uturuki wizara ya mambo ya kigeni mjini Berlin imesema Jumatatu, na kuongeza  tahadhari ya kusafiri kwenda Uturuki inaweza kutolewa iwapo ukamataji utaendelea.

https://p.dw.com/p/2jjYA
Sergey Elkin Karikatur Merkel EU-Türkeibeitritt

Msemaji  wa  wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Ujerumani  Martin Schaefer  amewaambia  waandishi  habari  kwamba  wizara  hiyo imepata  ishara  mahsusi  kwamba  Wajerumani  wawili , ambao  ni mke  na  mume  wake , wako  mikononi  mwa  polisi  tangu mwishoni mwa  juma.

Haifahamiki  watu  hao  wamekamatwa  kwa  sababu  gani, lakini Schaefer  ameongeza  kwamba  mmoja ameachiliwa  huru  na ameamriwa  kuondoka  nchini  humo.

Türkei Erdogans AKP feiert 16-jähriges Bestehen in Ankara
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/U. Bektas

"Hii  ina  maana jinamizi  kwa  Wajerumani  wengi  ambao  hawataki chochote  zaidi ya  kufurahia  mapumziko  yao  ya  likizo  nchini Uturuki linaendelea,"  amesema.

"Hali  hiyo  inaweza  kumuathiri  mtu  yeyote ambaye  ataamua kusafiri  kwenda  Uturuki.  Hutarajii  hatari  yoyote  na  ghafla unawekwa  jela, hilo  ni  jambo  la  huzuni  kabisa  ambalo tunakabiliana  nalo."

Schaefer  amesema  kutokana  na  hali  hiyo  ya  kigeugeu  ya maafisa  wa  Uturuki , Ujerumani inatafakari  kuiweka  Uturuki katika orodha ya  nchi zisizo faa  kwenda  hapo  baadae. "Iwapo hali  hii itaendelea  kuwa  ya  kila  siku  kwa  maafisa  wa  Uturuki kuwakamata  raia  wa  Ujerumani  mpakani  na  kuwaweka korokoroni , inawezekana  kwamba  wakati  utafika  kwamba  ushauri wa  kusafiri utatolewa,"  amesema.

Turkei Ankara - Angeklate werden zu Gericht gebracht
Baadhi ya watu waliokamatwa baada ya jaribio la mapinduzi ya mwaka 2016Picha: picture-alliance/abaca/Mustafa K.

Uhusiano wadhoofika

Uhusiano  kati  ya  Uturuki  na  Ujerumani umedhoofika  tangu  jaribio la  mwaka  jana  la  mapinduzi  dhidi  ya  rais Recep Tayyip Erdogan na  ukosoaji  mkali  wa  Ujerumani  uliosababishwa  na  ukandamizaji nchini  Uturuki ambao  umeshuhudia  zaidi  ya  watu  50,000 wakikamatwa. Mahusiano  yaliporomoka  zaidi  baada  ya kukamatwa  kwa  raia  kadhaa  wa  Ujerumani  ikiwa  ni  pamoja  na Deniz Yucel , mwandishi  habari  wa  gazeti  la  Die Welt.

Deutschland Bundeskanzlerin Angela Merkel und Recep Tayyip Erdogan in Hamburg
Angela Merkel (kushoto) na rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/POP-EYE/B. Kriemann

Wajerumani  11 wanashikiliwa  na  Uturuki  kwa  sasa  kwa  sababu za kisiasa, ikiwa  ni  pamoja  na  watatu  ambao  walikamatwa  tangu majira  ya  joto  mwaka  jana , kwa  mujibu  wa  wizara  ya  mambo ya  kigeni  ya  Ujerumani.

Wakati  huo  huo  kwa  mujibu  wa  waraka  uliotolewa  na  wizara ya  uchumi  ya  Ujerumani, na  kuonekana  na  shirika  la  habari  la Ujerumani dpa serikali  ya  Ujerumani  imeidhinisha  mauzo  ya silaha  nchini  Uturuki yenye  thamani  ya  euro  milioni 25  tangu mwanzo  wa  mwaka  huu 2017. Silaha 99 zilipokelewa  nchini Uturuki  zikiwa  na  thamani ya  euro milioni 25.36 ziliidhinishwa na serikali  ya  Ujerumani kati  ya  januari  na  Agusti , mwaka  huu , kwa mujibu wa  jibu  la  wizara  hiyo  kutokana  na  ombi  la  uhuru  wa kupata  taarifa  kutoka  chama  cha  upinzani  cha  kijani.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / dpae / rtre

Mhariri: Yusuf , Saumu