1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Uturuki erdogan awasili Ujerumani

Lilian Mtono
17 Novemba 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amewasili nchini Ujerumani kwa ajili ya ziara yake ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu, katikati ya sintofahamu kufuatia ukosoaji wake mkali dhidi ya Israel.

https://p.dw.com/p/4Z3C8
Picha inayomuonyesha kansela wa Ujerumani Olaf Scholz(kushoto) na Recep Tayyip Erdogan wa uturuki(kulia)
Kansela Olaf Scholz amekutana na rais Erdogan Novemba 17, 2023 wakati wakijaribu kuboresha uhusiano baina ya mataifa hayo, huku kukiwa na tofauti kuelekea vita vya Israel dhidi ya HamasPicha: INA FASSBENDER/AFP/Getty Images;Adem Altan/AFP/Getty Images

Rais Recep Tayyip Erdogan anazuru Ujerumani katikati ya sintofahamu baina ya mataifa hayo mawili, baada ya rais huyo kutoa matamshi makali kabisa ya kuikemea Israel kufuatia mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza, kiasi cha kuiita "taifa la kigaidi".

Erdogan amewasili katika uwanja wa ndege wa kijeshi nje ya mji mkuu Berlin muda mfupi uliopita kwa ajili ya ziara hiyo itakayodumu kwa masaa machache.

Viongozi mjini Berlin wamemkaribisha Rais huyo wa Uturuki kwa mazungumzo, katikati ya sintofahamu iliyochochewa na matamshi yake makali yaliyoitaja Israel kuwa ni "taifa la kigaidi" na kila wakati akiongeza ukosoaji wake dhidi ya Israel, tangu ilipoanzisha mashambulizi ya kisasi dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Ikumbukwe Hamas ilifanya shambulizi kubwa la oktoba 7, lililosababisha vifo vya karibu Waisrael 1,200, wengi wao wakiwa ni raia.

Kiongozi huyo wa Uturuki aidha ameishutumu Israel kwa uhalifu wa kivita, uliosababisha vifo vya watu 11,000 wengi wao wakiwa ni raia pamoja na watoto, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka zinazotawala Gaza.

Erdogan anazuru Ujerumani baada ya miaka mitatu

Msimamo huo wa Erdogan uliibua maswali mengi nchini Ujerumani kuhusiana na busara ya kumkaribisha wakati huu, huku upande wa upinzani wa kihafidhina na hata wa kiliberali, FDP ambao ni miongoni mwa unaounda serikali ya kansela Scholz , waliohoji kwa nini hakuifuta ziara hiyo?

Soma zaidi: Erdogan ahutubia maandamano ya kuiunga mkono Palestina

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiwa na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano wa kilele wa NATO
Pamoja na tofauti kati ya Ujerumani na Uturuki, lakini taifa hilo linasalia kuwa mshirika muhimu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na Ulaya Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Lakini msemaji wa Scholz Steffen Hebestreit amesema kumekuweko na mahusino mabaya baina ya washirika hao wawili ambayo wanalazimika kuyatafutia ufumbuzi, ingawa alikiri kwamba ni ziara ngumu na hasa kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.

Hii ni ziara ya kwanza ya Erdogan nchini Ujerumani tangu mwaka 2020, wakati alipohudhuria mkutano kuhusu Libya uliofanyika nchini humo.

Kwenye ziara hiyo Erdogan anatarajiwa kukutana na Rais wa shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier kwenye makazi yake rasmi Schloss Bellevue na kufanya mazungumzo, kabla ya baadae kukutana kwa mazungumzo na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz katika hafla ya chakula cha jioni.

Soma zaidi: Erdogan na Netanyahu wakutana kwa mara ya kwanza tangu mahusiano kuingia doa

Suala jingine ambalo huenda Erdogan akaliibua ni matarajio ya Uturuki ya kununua ndege 40 za kivita aina ya Eurofighter Typhoon, ambazo kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya Uturuki, mtengenezaji mwenza ambaye ni Ujerumani anapinga ununuzi huo.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili mara zote umekuwa mgumu, katika wakati ambapo Berlin ikikosoa vikali hatua kali za Erdogan dhidi ya wapinzani wake wa ndani. Lakini hata hivyo bado Uturuki bado anasalia kuwa mshirika muhimu si tu kwa Ujerumani bali pia Ulaya na Jumuiya ya kujihami ya NATO, na hasa kutokana na ushiriki wake kuanzia kusimamia makubaliano ya usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine katikati ya vita vya Urusi hadi makubaliano muhimu ya kudhibiti mmiminiko wa wahamiaji barani Ulaya kati ya mwaka 2015-16.

Erdogan anatarajiwa kurejea Uturuki kesho usiku wa leo.