1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuongeza mbinyo mapambano ya COVID-19

Admin.WagnerD15 Oktoba 2020

Kansela Angela Merkel na viongozi wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani wamekubaliana kuongeza makali ya amri ya kuvaa barakoa pamoja na kufungwa mapema maduka ya kuuza pombe katika maeneo yenye visa vingi vya COVID-19.

https://p.dw.com/p/3jxET
Berlin Merkel bei Nationaler Integrationspreis
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mkutano uliofanyika jana saa chache tangu Ujerumani iliporipoti maambukizi mapya  5,000 ya virusi vya corona katika kipindi cha saa 24, kiwango ambacho kikubwa kuwahi kushuhudiwa tangu katikati ya mwezi April.

Mapendekezo yaliyotolewa yanataka amri ya kuvaa barakoa ambayo tayari ni lazima ndani ya vyombo vya usafiri na maduka nchini Ujerumani pia itekelezwe kwenye maeneo ya umma yaliyo na msongamano katika wilaya zenye maambukizi makubwa ya  COVID-19.

Wakati hali nchini Ujerumani bado inatia moyo ikilinganishwa na mataifa mengine barani Ulaya, Kansela Merkel amesema ni muhimu kupunguza kwango cha maambukizi.

"Ninashawishika kuwa kile tutafanya au kutofanya katika siku na wiki zinazokuja kitakuwa muhimu kwa jinsi tutaondokana na janga hili. Kwa sabababu tunaweza kuona tarakimu za maambukizi ziko juu , baadhi ya maeneo kiwango kiko juu kabisa na pia tuna kiwango cha juu sana cha maambukizi katika baadhi ya majimbo ya Ujerumani ".

Miji mingi ya Ujerumani ikiwemo, Berlin, Cologne, Dusseldorf, Frankfurt na Munich imeshuhudia wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona hatua iliyolazimisha kurejeshwa kwa vizuizi vya kuzuia kusambaa virusi hivyo.

Ufaransa yatangaza marufuku ya kutoka nje 

Präsident Macron im TV zur Corona-Krise
Rais Emmanuel Macron wa UfaransaPicha: Alexandre Marchi/Maxppp/dpa/picture alliance

Wakati hayo yakijiri nchini Ujerumani, taifa jirani la Ufaransa limetangaza kuwa siku ya Jumamosi litaanza kutekeleza marufuku ya kutoka nje usiku kwenye mji mkuu Paris na miji mingine 8 mikubwa katika juhudi zake za kukabiliana na janga la virusi vya corona.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, rais Emannuel Macron wa Ufaransa amesema marufuku hiyo itakuwa kati ya saa tatu usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi na itumudu kwa hadi muda wa wiki sita.

Macron amesema lengo la hatua hiyo ni kupunguza maambukizi ya COVID-19 kutoka wastani wa sasa wa visa 20,000 kwa siku hadi angalau visa 3,000 au 4,000 idadi ambayo inaweza kudhibitiwa.

Mataifa masikini yapata afueni 

Deutschland Videokonferenz Scholz Finanzminister G20
Picha: Reuters/H. Hanschke

Kwengineko mataifa ya kundi la G20 yamekubaliana kurefusha kwa miezi sita muda wa kulipa madeni kwa mataifa maskini yaliyoathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona .

Wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya video, mawaziri wa fedha na magavana wa kundi la G20 wameridhia kusogeza mbele hadi Juni 2021 kuwa muda wa mwisho kwa mataifa masikini kuanza tena kulipa madeni yake

Usimamishaji wa kulipa madeni ulikuwa unafikia tamati mnamo mwezi Novemba mwa huu na kundi la G20 limesema muda wa nyongeza uliokubaliwa jana unaweza kurefushwa tena wakati wa majadiliano yatafanyika wakati wa majira ya kiangazi mwaka 2021.