1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa ECOWAS waenda Mali kuendeleza usuluhishi

Daniel Gakuba
22 Agosti 2020

Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan anaongoza ujumbe wa jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, kuzungumza na wanajeshi waliofanya mapinduzi, pamoja na rais aliyepinduliwa, Ibrahim Boubacar Keita.

https://p.dw.com/p/3hLO4
Mali Putsch Pressekonferenz
Ismael Wague (katikati), msemaji wa kundi la wanajeshi walioiangusha serikali ya MaliPicha: picture-alliance/dpa

Wapatanishi kutoka jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wanakwenda nchini Mali, katika mazungumzo yenye azma ya kubatilisha mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini humo mwanzoni mwa wiki hii.

Mapinduzi hayo yaliyomuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita yalilaaniwa na jumuiya ya kimataifa, lakini yalishangiliwa katika nchi hiyo inayokabiliwa na uasi wa kijihadi pamoja na mtafaruku wa kisiasa.

ECOWAS yenye nchi 15 wanachama imechukua msimamo mkali dhidi ya wanajeshi walioiangusha serikali ya rais Keita, kwa kuifunga mipaka ya nchi hiyo na kuzuia mtiririko wa fedha kuingia Mali.

Mwenzako akinyolewa......

Wanadiplomasia wanashuku hatua za viongozi wa jumuiya hiyo  zinalenga zaidi kuwaogofya wapinzani wa nyumbani kuliko utulivu nchini Mali.

Krise in Mali | ECOWAS | Goodluck Jonathan und Boubou Cissé
Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan (kushoto) ndiye anayeongoza ujumbe wa ECOWAS nchini Mali.Picha: Présidence du Mali

Mmoja wa wanadiplomasia hao amesema ''wanatazama kinachotokea Mali na kujifiria wao, huenda zamu inayofuata ni yao, na hilo hawawezi kulivumilia.''

Marais wa Ivory Coast na Guinea ni miongoni mwa wale wanaopigia debe vikwazo vikali dhidi ya wanajeshi waliofanya mapinduzi Mali, na kulingana na mwanadiplomasia mwingine, wote wawili wamekabiliwa na upinzani wa umma dhidi ya uamuzi wao wa kuwania muhula wa tatu madarakani.

Macho yote yataelekezwa katika ujumbe huo wa ECOWAS unaoongozwa na rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan, ambaye kulingana na taarifa ya msemaji wake, wanawasili jioni hii katika mji mkuu wa Mali, Bamako. Afisa mmoja anayeshiriki katika ujumbe huo amesema wataweza kukutana na rais aliyepinduliwa, Ibrahim Boubacar Keita.

Kazi ngumu kumrejesha Ibrahim Boubacar Keita mamlakani

Mali | Präsident Ibrahim Boubacar Keita
Ibrahim Boubacar Keita, rais wa Mali aliyepinduliwa na wanajeshiPicha: Getty Images/AFP/L. Marin

Kupinduliwa kwa Rais Ibrahim Boubacar Keita kulikaribishwa kwa shangwe na wananchi wengi wa Mali, ambao kwa miezi kadhaa iliyopita wamekuwa wakiteremka majiani kumshinikiza aachie madaraka, kutokana na kashfa za ubadhirifu na kuyumba kwa usalama katika maeneo yaliko makundi ya kijihadi kama al-Qaida na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

''Kumrejesha madarakani Ibrahim Boubakar Keita ni kitu kisichowezekana'', amesema mwanadiplomasia mmoja kutoka Afrika Magharibi, na kuongeza kuwa kinachowezekana tu, ni kuundwa kwa serikali ya mpito. Kwa mujibu wa kanuni za ECOWAS, amesema mwanadiplomasia huyo, jumuiya hiyo inapaswa kupewa jukumu la kuisimamia serikali hiyo.

Hayo yakiarifiwa, wanajeshi wanne wa jeshi la Mali wameuawa katika mripuko a bomu la kutegwa kando ya barabara katika eneo la katikati mwa nchi, na mwingine mmoja amejeruhiwa vibaya katika shambulio hilo.

 

RTRE, AFP