1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya bado iko katika mkwamo kuunusuru uchumi wake

20 Julai 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamefanya majadiliano hadi Jumatatu alfajiri kujaribu kupata suluhisho wakati ambapo mkutano wao wa kilele wa mpango wa kuufufua uchumi baada ya virusi vya corona ukiwa unaingia siku ya nne.

https://p.dw.com/p/3fZw3
Brüssel I EU-Gipfel I Tag 3 I Charles Michel I Emmanuel Macron I Angela Merkel I Ursula von der Leyen
Picha: Reuters/F. Francois Walschaerts

Kulikuwa na hamaki na kukata tamaa katika chumba cha mkutano huo baada ya wikendi nzima ya majadiliano huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwashambulia viongozi wa Uholanzi na Austria na kutishia kuondoka kwenye kikao hicho.

Mazungumzo hayo yasiyokuwa na mapumziko yaliyochini ya uenyekiti wa Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel yameshindwa kuleta makubaliano kuhusiana na kiwango na masharti katika kugawanya yuro bilioni 750 miongoni mwa nchi za Ulaya ili kusaidia kuunusuru uchumi wa bara hilo uliporomoka kutokana na janga la virusi vya corona. Lakini Michel amewataka viongozi hao kujaribu kutafuta suluhu kwa mara ya mwisho.

EU-Sondergipfel zur Bewältigung der Corona-Wirtschaftskrise
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles MichelPicha: picture-alliance/dpa/AP/Reuters Pool/F. Lenoir

Hatuezi kukubali kiholela holela

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte ameituhumu Uholanzi na marafiki zake Sweden, Denmark, Finland na Austria kwa kuziendea kinyume nchi zengine katika Umoja wa Ulaya. Lakini Kansela wa Austria Sebastian Kurz amesema watashikilia msimamo wao.

"Hili ni suala muhimu sana kwasababu naamini kwamba hatuwezi tu kukubali kiholela holela. Kuna kiwango flani cha uwezekano wa kubadilisha msimamo katika nchi nyingi ila sisi tumekubaliana tutashikilia msimamo wetu ambao uko wazi na hatuko tayari kwenda chini ya kiwango fulani. Hilo bila shaka litalazimu mijadala mingine kufanyika," alisema Kurz.

Kuna uwezekano wa mkutano kusitishwa bila suluhisho

Wanadiplomasia wanasema huenda viongozi hao wakasitisha mkutano huo na kujaribu tena kupata makubaliano mwezi ujao. Na kutokana na hofu hiyo ya kusitishwa kwa mkutano bila makubaliano kupatikana, Michel amependekeza pesa zitakazotolewa kwa nchi bila malipo ziwe yuro bilioni 400 kinyume na pendekezo lake la awali la yuro bilioni 500 na akaongeza pendekezo lake la mkopo kutoka yuro bilioni 250 hadi yuro bilioni 350.

Brüssel I EU-Gipfel I Tag 3 I Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Getty Images/AFP/J. Thys

Rais wa Benki Kuu ya Ulaya Christine Lagarde amesema ni bora viongozi hao wakubaliane kutoa msaada wa fedha kwa nchi kuliko kupata suluhu la haraka kwa gharama yoyote.

Mazungumzo hayo yameonyesha wazi mpasuko ulioko kati ya nchi za Umoja wa Ulaya zilizo kaskazini mwa bara hilo na zile za kusini.