1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yaitaka Kenya itangaze tarehe ya uchaguzi

1 Julai 2011

Umoja wa Ulaya umeitaka serikali ya Kenya kutangaza siku ya uchaguzi ujao wa nchi hiyo na ipitishe sheria kabla ya hapo, ili kuepusha kurudiwa tena kwa machafuko baada ya uchaguzi wa mwaka 2004 nchini humo.

https://p.dw.com/p/RX4K
Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru KenyattaPicha: AP

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya kwa Kenya, Lodewijk Briet, alisema hapo jana (30.07.2011) kwamba kumekuweko maendeleo katika marekebisho ya kisiasa na kimahakama, lakini mengi zaidi yanahitajika kufanyika ili kuhakikisha uchaguzi ujao utakuwa wa amani.

Briet alisema kuna hatari ya Kenya kupoteza nia njema ya kimataifa na huenda fedha zaidi kwa ajili ya kuleta marekebisho, ikiwa nchi hiyo itakwenda polepole katika kuitekeleza katiba.

Umoja wa Ulaya umekuwa, kwa sehemu, ukigharamia mwenendo wa kuleta marekebisho katika nchi hiyo.

Mawazo yanagawika miongoni mwa wabunge wa Kenya na ile tume ya kuitekeleza katiba juu ya lini uchaguzi ujao uitishwe, na kumekuweko mdahalo miongoni mwa wananchi kuhusu jambo hilo, lakini hamna uamuzi rasmi uliofikiwa.

Viongozi wa Umoja wa Afrka wakutana tena kuhusu Libya

Bendera za mataifa ya Afrika mbele ya makao makuu ya Umoja wa Afrika, Addis Ababa
Bendera za mataifa ya Afrika mbele ya makao makuu ya Umoja wa Afrika, Addis AbabaPicha: picture-alliance/landov

Viongozi wa Umoja wa Afrika wamekutana tena leo hii kuweka sawa vipengee muhimu katika mpango wa amani kukomesha mzozo wa Libya huku kukiwa na shinikizo kutoka kwa waasi Libya kutaka kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, aondoke madarakani.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika, Jean Ping, ameliambia Shirika la Habari la AFP kwamba hilo ni suala muhimu na leo ni siku muhimu wakati wakuu wa nchi wakiwa wamewasili kuanza tena mazungumzo ya faragha ambayo yalifunjika mapema leo asubuhi bila ya kufikia makubaliano.

Waasi wa Libya warudishwa nyuma

Waasi wa Libya wakifurahia ushindi wa 'muda'
Waasi wa Libya wakifurahia ushindi wa 'muda'Picha: dapd

Waasi wa Libya wamerejea nyuma hii leo kutoka vituo vyao nje ya mji wa Bir al-Ghanam, umbali wa kilomita 80 kusini mwa mji mkuu, Tripoli, baada ya kushambuliwa kwa makombora la jeshi la serikali. Hayo ni kwa mujibu wa ripota wa Shirika la Habari la Uengereza, Reuters.

Ripota huyo ameongeza kusema vikosi vya serikali vilivyoko Bir al Ghanam vimewavurumishia waasi makombora yaliyotengenezwa Urusi, yaliyopiga kilomita 30 kusini mwa mji huo.

Bashir arudi Sudan

Rais Omar al-Bashir (kushoto) na Rais wa China Hu Jintao
Rais Omar al-Bashir (kushoto) na Rais wa China Hu JintaoPicha: AP

Rais Omar al Bashir, anayeandamwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za kuhusika na mauwaji ya halaiki, amerejea Khartoum leo baada ya ziara ya siku tatu katika Jamhuri ya Umma wa China.

Shirika la Habari la Sudan (SUNA) limemnukuu Rais Bashir akisema kuwa mazungumzo yake pamoja na viongozi wa China yalihusiana na namna ya kuzidishwa shughuli za kuchimba mafuta nchini Sudan, masuala ya kilimo na madini.

Sudan na China zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na teknolojia. SUNA imesema kuwa ziara hiyo imelenga kuhakikisha hakutokuweko mabadiliko yoyote katika siasa ya China kuelekea Sudan baada ya Sudan ya Kusini kujipatia uhuru wake hapo Julai 9, 2011.

Tanzania itajenga barabara ya Serengeti

Msafara wa Nyumbu katika mbuga ya Serengeti
Msafara wa Nyumbu katika mbuga ya SerengetiPicha: picture alliance/dpa

Tanzania bado inapanga kujenga barabara kuu kupitia njia ya mbuga ya wanyama ya Serengeti. Hayo yalisemwa na Waziri wa Utalii na Maliasili wa nchi hiyo, Ezekiel Maige, akilikanusha tangazo la Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwamba mradi huo umetupiliwa mbali.

Maige amesema serekali itaendelea na mradi huo, lakini kuachilia kilomita 120 katika mbuga hiyo kwa ajili ya barabara ya changarawe. Alisema barabara hiyo ya changarawe haitakuwa na athari kubwa kwa wanyama pori. B

Maige alielezea kwamba sehemu za barabara hiyo itakayopita katika mbuga hiyo maarufu hazitawekewa lami. Alizitaja sehemu hizo ni za urefu wa kilimota 12 kutoka Mugumu hadi Tabora B na ile ya urefu wa kilomita 57 kutoka Tabora B kupitia Lango la Klens hadi Loliondo.

Jumamosi iliyopita, afisa wa shirika la UNESCO aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba Kamati ya Turathi ya Shirika hilo imepata uhakikisho kutoka serekali ya Tanzania kwamba mradi huo wa barabara kuu umeachwa.

Mwandishi: Mohammed Dahman

Mhariri: Othman Miraji