1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika wanaendelea na mkutano Malabo

Halima Nyanza30 Juni 2011

Mkutano wa Viongozi wa Afrika leo umeingia siku ya pili, wakati viongozi hao wanatafuta uungwaji mkono mpango wa kuumaliza mzozo wa Libya

https://p.dw.com/p/11mE8
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/ dpa

Wajumbe wa kundi la waasi nchini Libya walioalikwa kwenye mkutano huo mjini Malabo Guinea ya ikweta, waliendelea kusisitiza kuwa kiongozi wa Libya Muammer Gaddafi ajiuzulu.

Mkutano huo wa Umoja wa Afrika ulianza hapo jana kukiwa tayari na mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wake, ambao baadhi wamekuwa wakimuunga mkono kiongozi huyo aliyeitawala Libya kwa muda mrefu kutokana na kulifadhili kwake bara la Afrika kwa mambo mbalimbali kuanzia kutatua mizozo mpaka maendeleo, na kwamba Gaddafi aliwahi kushika wadhfa wa uenyekiti wa umoja huo miaka miwili tu iliyopita.

Lakini hata hivyo wengine wanasema muda umefika kwa yeye kung'atuka.

Mmoja ya wajumbe anayehudhurika mkutano huo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema hakuna anayetaka kusema wazi, kwasababu Gaddafi amewasaidia sana kifedha.

Libya yenyewe katika mkutano huo imewakilishwa na pande zote mbili, wawakilishi toka serikalini na pia waasi.

Waziri wa Libya anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Afrika, Joma Ibrahim Amer, aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mkutano huo, kwamba serikali ya Gaddafi inatarajia kuungwa mkono na Umoja wa Afrika.

Amesema msimamo wa Umoja wa Afrika uko wazi kabisa, ambapo mpango wake wa kupatikana kwa ufumbuzi wa mzozo huo kwa amani, unaungwa mkono na Libya.

Amesisitizia kuwa mpango huo ni hatua muhimu katika kupatikana ufumbuzi wa amani, lakini mashambulio yanayofanywa na jeshi la Jumuia ya Kujihami ya NATO ambayo yanalenga maeneo ya raia kama vile shule na hospitali, lazima kwanza yasitishwe.

Aidha Waziri huyo wa Libya amesema nchi yake haitambui waranti uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita wiki iliyopita, ya kukamatwa kwa Gaddafi, mtoto wake Saif al Islam na mkuu wa Usalama wa taifa wa nchi hiyo kwa makosa dhidi ya uhalifu wa binadamu.

Ameishutumu mahakama hiyo kwa kutumiwa kama chombo cha kisiasa na mataifa makubwa, hususan dhidi ya nchi za Kiafrika, akitolea mfano waranti mwingine uliotolewa na mahakama hiyo dhidi ya Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir.

Akizungumzia hatua hiyo ya ICC, Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean Ping, amesema inasababisha hali kuwa ngumu zaidi.

Kwa upande wao waasi, ambao pia wametuma ujumbe wao katika mkutano huo wa Malabo, wameshasema wazi kwamba wataunga mkono tu, mpango wa Umoja wa Afrika utakaowezesha Gaddafi kuondoka madarakani.

Mkutano huo umeanza hii leo baada ya jopo la viongozi lililo na jukumu la kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo wa Libya, kukutana jana usiku, huku pendekezo lao la ufumbuzi wa kisiasa katika mzozo huo wa Libya lililojikita katika mpango wao ulioandaliwa mwezi Machi, likitarajiwa kuwasilishwa, ili kuweza kuungwa mkono.

Jopo hilo linalowajumuisha marais watano, akiwemo Jacob Zuma wa Afrika ya kusini na Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania jana pia lilijadili hali inavyoendelea nchini Libya tangu, walipokutana mara ya mwisho, wiki iliyopita.

Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama katika umoja wa Afrika Ramtane Lamamra amesema jopo hilo ambalo pia linawahusisha rais Yoweri Musseveni wa Uganda, Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo pamoja na rais wa Mali Amadou Toumani Toure, limezingatia uchaguzi kuchagua "ufumbuzi wa amani".

Kauli mbiu ya mkutano huo wa Umoja wa Afrika ni "Vijana na maendeleo".

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)
Mhariri: Mtullya abdu