1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kuijadili Libya

Grace Kabogo
6 Januari 2020

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kuijadili Libya wakati ambapo wanajeshi wa Uturuki wameanza kupelekwa Libya katika juhudi za kuiunga mkono serikali ya Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/3Vkje
UN-Weltsicherheitsrat tagt zum Libyen-Konflikt
Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/Li Muzi

Wanadiplomasia wamesema kuwa mkutano huo wa faragha unaofanyika kutokana na ombi la Urusi, utatoa nafasi kwa mara ya kwanza kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadiliana kuhusu mikataba yenye utata ya usalama na shughuli za baharini ambayo ilisainiwa kati ya Libya na Uturuki mwezi Novemba.

Mikataba hiyo ilizikasirisha nchi nyingine zinazotumia Bahari ya Mediteranea ikiwemo Ugiriki na Cyprus, ambayo pia inatafuta kutumia rasilimali za nishati katika ukanda huo, ambapo hifadhi ya gesi imegunduliwa hivi karibuni. Mkutano huo unalenga rasmi mijadala ya kimataifa kuhusu Libya ambayo Ujerumani ina matumaini ya kuandaa hadi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu. Hadi sasa hakuna tarehe iliyotangazwa kwa ajili ya mkutano huo.

Türkei l Erdogan will Truppen nach Libyen schicken - Militär
Majeshi ya UturukiPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Mkutano huo pia utaijadili hatua ya Uturuki kupeleka wanajeshi wake nchini Libya. Uturuki imeufikia uamuzi huo baada ya serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Tripoli inayoongozwa na Fayez al-Sarraj, kuomba rasmi msaada wa kijeshi kutokana na jeshi linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi mwezi Aprili.

Wanajeshi waanza kwenda Libya

Jana Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alitangaza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wameanza kupelekwa Libya, baada ya bunge kuidhinisha hatua hiyo wiki iliyopita.

''Kazi ya wanajeshi wetu huko ni kuratibu. Wataanzisha kituo cha operesheni nchini Libya, ambako luteni jenerali wa Kituruki atakiongoza na wataisimamia hali ya huko. Wanajeshi wetu wanakwenda Libya hatua kwa hatua. Tutakuwa na vitengo tofauti vitakavyofanya kazi kama vikosi vya mapambano,'' alifafanua Erdogan.

Erdogan amebainisha kuwa lengo lao sio kupigana, bali kuiunga mkono serikali halali na kuzuia mzozo wa kibinaadamu. Haftar anaungwa mkono na wapinzani wa kikanda wa Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri, huku serikali ya Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa ikiungwa mkono na Uturuki pamoja na mshirika wake Qatar.

Kombibild - Erdogan, Khalifa Haftar, Fajis al-Sarradsch
Jenerali Khalifa Haftar, Rais Recep Tayyip Erdogan na Fayez al-Sarraj

Wanadiplomasia ambao hawakutaka kutajwa majina yao wamesema hawana uhakika kama kuna uwezekano kwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzungumzia suala la mamluki wa Urusi wanaomsaidia Haftar. Urusi imekanusha kuhusika katika mapambano hayo.

Ijumaa iliyopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alirejea wito wake wa kutaka mapigano nchini Libya yasitishwe mara moja. Guterres alisema msaada wowote wa nchi za kigeni kwa pande zinazohasimiana utaongeza tu mzozo unaoendelea na kuzifanya juhudi zilizopo za kupata suluhisho kamili la kisiasa kwa njia ya amani kuwa ngumu zaidi.

Katika hatua nyingine serikali ya libya imesema kuwa watu wapatao 30 waliuawa na wengine 33 walijeruhiwa katika shambulizi la anga lililotokea kwenye shule moja mjini Tripoli Jumamosi iliyopita.

(AFP, DPA, Reuters)