1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya raia Syria

4 Agosti 2011

Baada ya siku kadhaa za kushindwa kufikia uamuzi hatimaye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limetoa tamko la kulaani hatua ambazo serikali ya Syria inachukua kukabiliana na waandamanaji wanaoipinga serikali hiyo.

https://p.dw.com/p/12Axk
Rais wa Baraza la Usalama, Balozi wa India katika Umoja wa Mataifa Hardeep Singh PuriPicha: picture alliance/dpa

Tamko hilo limetolewa huku maelfu ya waandamanaji kwa mara nyingine wakiingia mitaani huko katika mji wa Hama pamoja na kuendelea kuwepo kwa vifaru na wanajeshi mjini humo.

Baraza hilo katika taarifa yake limesema kuwa suluhisho pekee la mzozo huo ni kwa serikali ya Rais Bashar Assad kushirikiana katika mchakato wa kisiasa ambao utatambua uhalali wa matakwa ya wananchi wa nchi hiyo.

Akisoma taarifa hiyo, Balozi wa India katika Umoja wa Mataifa ambaye ndiye rais wa baraza hilo, Hardeep Singh Puri, amesema Umoja wa Mataifa unalaani vifo vya raia na kutaka wale wote wanaohusika na ghasia hizo kuwajibika.

"Baraza la Usalama linaelezea wasiwasi wake mkubwa na kuendelee kuzorota kwa hali nchini Syria na linasikitishwa sana na vifo vya mamia ya watu. Baraza la Usalama linalaani kuendelea kwa uvunjani wa haki za binaamu, na matumzi ya nguvu dhidi ya raia yanayofanywa na serikali ya Syria"alisema.

Mara baada ya kusomwa kwa taarifa hiyo Lebanon ilisema haiungi mkono taarifa hiyo na kwamba inasimama bega kwa bega na serikali ya Syria.Balozi wake kwenye umoja wa mataifa alinukuliwa akisema hakupiga kura.

Hata hivyo Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa lilishindwa kukubaliana juu ya azimio. Mataifa ya Magharibi yalikuwa na matumaini ya kupitishwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali inayoendelea huko Syria, lakini yamepingwa na China na Urusi ambazo zina kura ya turufu.

Nchi hizo mbili zina hofu kuwa kupitishwa kwa azimio dhidi ya Syria kunaweza kufungua njia ya kuingilia kijeshi mzozo. Lakini Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin alisema walishiriki kikamilifu.

´´Tunasikitishwa na vurugu pamoja na kuendelea kwa mzozo huu, na tunadhani kwamba katika mazingira haya, baraza la usalama, linaweza na ni lazima litoe ishara endelevu ambayo ni kutumia siasa kuumaliza mzozo huo, na sisi tumeshiriki kikamilifu na nia nzuri katika majadiliano kwenye baraza la usalama´´

Lakini Naibu wa Balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa Miguel Berger amesema taarifa hiyo ni ishara tosha kuwa wanachama wanaguswa na kile kinachoendelea Syria.

"Nadhani ni wazi hii ni hatua moja mbele ya kwamba wanachama wote wa baraza hili wameshiriki katika majadiliano makali. Hilo pekee linatoa ishara kuwa kuna wasiwasi mkubwa katika baraza la usalama kuhusiana na kudorora kwa hali nchini Syria"

Hiyo ni taarifa ya kwanza ya Umoja wa Mataifa kulaani hali nchini Syria tokea kuzuka kwa upinzani dhidi ya Rais Bashar al Assad katikati ya mwezi Machi mwaka huu. Baraza la Usalama limemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Ban Ki-moon kuliarifu baraza hilo juu ya hali itakavyokuwa ikiendelea huko Syria mnamo kipindi cha siku saba zijazo.

Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binaadamu zaidi ya watu 1,500 wamekwishauawa tokea kuanza kwa upinzani huo. Kwa upande wake serikali ya Syria imesema mamia ya askari wake wameuawa.

Taarifa hiyo imetolewa huku mamia ya vifaru na wanajeshi wa Syria wakiendelea kubakia katikati ya mji wa Hama na mji wa Deir Ezzor.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/Reuters/ZPR

Mhariri:Josephat Charo