1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa washindwa kuidhinisha azimio la Palestina

31 Desemba 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kupitisha azimio la kuitaka Israel kuacha kulikalia kwa mabavu eneo la Ukingo wa Magharibi ifikapo Disemba 31, mwaka 2017 pamoja na kuruhusu Palestina kuwa taifa huru.

https://p.dw.com/p/1EDQD
Bendera ya Palestina
Bendera ya PalestinaPicha: picture-alliance/dpa/I. Langsdon

Ufaransa, Urusi na China ni miongoni mwa nchi nane zilizopiga kura kuliunga mkono azimio hilo, lakini Marekani na Australia wamepiga kura ya kulipinga. Nchi nyingine tano ikiwemo Uingereza, hazikupiga kura.

Balozi wa Jordan kwenye Umoja wa Mataifa, Dina Kawar, amesema hiyo ni haki halali ya watu wa Palestina ambayo wameichagua katika juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power, amesema wamepiga kura kulipinga azimio hilo siyo kwa sababu wanaridhishwa na hali iliyopo, bali kwa sababu amani inapaswa kupatikana kwa njia ya mazungumzo ya maafikiano.

Balozi wa Marekani, Samantha Power
Balozi wa Marekani, Samantha PowerPicha: Burton/Getty Images

Siku ya Jumatatu mataifa 22 ya Kiarabu yakiwakilishwa na Jordan kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yalikubali kuliunga mkono pendekezo la Palestina kuhusu marekebisho ya azimio la Umoja wa Mataifa la kutaka Israel kuacha kuikalia kimabavu Palestina katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Power ameukosoa uamuzi wa kupelekwa kwa muswada wa azimio hilo kwa ajili ya kupigiwa kura na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa kuwa halitazikutanisha pamoja kwa karibu pande zinazohasimiana.

Palestina yasema ujumbe wao umekataliwa

Balozi wa Palestina kwenye umoja huo, Riyad Mansour amesema ujumbe wao ulikuwa ni juhudi kubwa na zenye uhalisia kwa ajili ya kufungua mlango wa amani, lakini kwa bahati mbaya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haliko tayari kuusikiliza ujumbe huo.

Muda mfupi kabla ya kura hiyo, wanadiplomasia wa baraza hilo walitarajia azimio hilo litapata kura tisa za ''ndiyo'', lakini Nigeria ambayo inaaminika kuliunga mkono azimio hilo, haikupiga kura. Balozi wa Nigeria kwenye Umoja wa Mataifa, Joy Ogwu, ameunga mkono msimamo wa Marekani akisema kuwa njia ya mwisho ya amani inaegemea katika suluhisho la mazungumzo.

Balozi wa Palestina, Riyad Mansour
Balozi wa Palestina, Riyad MansourPicha: picture alliance/AP Photo

Marekani, ambayo ni mwanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mshirika wa karibu wa Israel, imesema pendekezo hilo la Palestina halina manufaa. Siku ya Jumatatu, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Jeff Rathke aliwaambia waandishi wa habari kwamba azimio hilo jipya siyo jambo ambalo wanaweza wakaliunga mkono na kwamba nchi nyingine zina mtazamo sawa na Marekani.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema iwapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haitolikataa azimio hilo, wao watalipinga. Amesema mamlaka ya Palestina inajaribu kuweka amri kwa Israel ambayo itadhoofisha usalama wa Israel na kuuweka mustakabali wake wa baadaye katika hatari. Amesema Israel itayapinga mazingira yoyote yatakayohatarisha maisha yake ya baadaye.

Wasiwasi kuhusu kuzuka mvutano kati ya Israel na Palestina umeongezeka baada ya mazungumzo ya amani kushindikana mwezi Aprili mwaka huu, hali iliyosababisha kuanza kwa mashambulizi wakati wa majira ya joto yaliyowaua maelfu ya Wapalestina.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE, APE
Mhariri: Mohamed Khelef