1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wasikitishwa na mzozo wa Tigray

Lilian Mtono
23 Aprili 2021

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limeelezea wasiwasi mkubwa juu ya kusambaa kwa visa vya ukiukwaji wa haki za binaadamu katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

https://p.dw.com/p/3sT16
USA Sicherheitsrat der Vereinten Nationen Friedensverhandlungen in Kolumbien
Picha: picture-alliance/dpa/M. Rajmil

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limeelezea wasiwasi mkubwa juu ya kusambaa kwa visa vya ukiukwaji wa haki za binaadamu katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia, hiyo ikiwa ni taarifa yake ya kwanza tangu kulipozuka mzozo kwenye eneo hilo November mwaka 2020. 

Tamko hilo lililoandaliwa na Ireland na kukubaliwa na wanachama wote 15 wa baraza hilo imeelezea wasiwasi mkubwa kuhusiana na madai ya kukiukwa kwa haki za binaadamu na unyanyasaji, na kutoa mwito wa uchunguzi ili kuwatambua wahusika na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria.

Soma Zaidi: Umoja wa Mataifa wakubali uchunguzi wa pamoja Tigray

Aidha baraza hilo la usalama limetoa mwito wa kuimarishwa kwa juhudi za kufikisha misaada ya kiutu kwa watu wote wenye mahitaji, na kurejea kauli yake ya kusaidia juhudi za kikanda na eneo zima la kusini mwa Afrika katika kusuluhisha mzozo huo.

Visa vya ukiukwaji vinavyoripotiwa ni pamoja na unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana. Tamko hili linatolewa wiki moja baada ya mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa kusema unyanyasaji wa kingono ulikuwa ukitumika kama silaha ya vita kwenye jimbo la Tigray.

BG Tigray | Safe House
Mamia ya wanawake wamebakwa na kusahmbuliwa kingono na wanajeshi tangu kulipozuka mzozo jimboni Tigray.Picha: Maria Gerth-Niculescu/DW

Mwezi uliopita, baraza hilo halikufikia makubaliano kuhusiana na lugha iliyotumika kwenye taarifa hiyo wakati kulipoibuka mvutano kati ya mataifa ya Magharibi dhidi ya Urusi na China ambao mabalozi wake walihoji kuhusiana na iwapo baraza hilo lenye jukumu la kuimarisha amani na usalama ulimwenguni, linatakiwa kuhusishwa.

Mkurugenzi wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu Robert Mardini alipozungumza kutokea Geneva, Uswisi amesisitiza kwa kusema hali inatia wasiwasi na wanasikia visa vibaya mno, ambavyo hawajavisikia kwa zaidi ya miongo miwili.

"Ripoti hizo ni za kutisha sana, za kushangaza sana. Sijasikia visa vibaya kama hivyo kwa zaidi ya miongo miwili katika eneo la masuala ya kibinaadamu. Wenzangu wengi wanashuhudia vivyo hivyo, kwa hivyo hiki ni kipaumbele chetu, kuzuia haya kutokea tena na kwa kweli kufanya kila tuwezalo kuwasaidia wahanga." amesema Mardini.

Mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock wiki iliyopita aliliambia baraza hilo kwamba mzozo wa kibinaadamu katika jimbo la Tigray umezidi kuongezeka, wakati kukishuhudiwa changamoto za kufikisha misaada, watu wakiwa wanakufa kwa njaa huku pia kukiwa na ripoti za ubakaji wa makundi, ambapo kundi la wanaume humshambulia mhanga mmoja, na katika baadhi ya matukio wanawake wamekuwa wakibakwa mara kadhaa. Alisema, wasichana wa hadi miaka minane wamekuwa wakilengwa.

Soma Zaidi: Umoja wa Mataifa wafadhaishwa na taarifa za vitendo vya ubakaji katika jimo la Tigray

Ujumbe wa Ethiopia kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York ulisema kwenye taarifa yake jana kwamba operesheni ya kijeshi nchini humo ni suala la ndani linalosimamia na sheria za nchi hiyo, ambazo ni pamoja na za haki za binaadamu.

Mashirika: RTRE/AFPE