1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa watishia kuwekea Sudan Kusini vikwazo

John Juma
1 Juni 2018

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limezipa pande hasimu nchini Sudan Kusini muda wa mwezi mmoja kufikia makubaliano ya amani la sivyo wawekewe vikwazo

https://p.dw.com/p/2ymvs
UN-Sicherheitsrat
Picha: picture-alliance/Photoshot/Li Muzi

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limezipa pande hasimu nchini Sudan Kusini muda wa mwezi mmoja kufikia makubaliano ya amani la sivyo wawekewe vikwazo. Mswada wa azimio hilo ulioandaliwa na Marekani, ulipata ushindi mdogo wa kura 9 katika baraza hilo lenye nchi wanachama 15. Nchi 6 zikiwemo China, Urusi na Ethiopia ambazo ni washirika muhimu katika juhudi za kutafuta amani ya eneo hilo hazikupiga kura.

Azimio hilo linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kuwasilisha ripoti ifikapo Juni 30, kueleza ikiwa makubaliano yaliofikiwa mwezi Disemba yanatekelezwa na ikiwa pande husika zimepata suluhisho muafaka la kisiasa kusitisha mapigano.

Ikiwa makubaliano hayo ambayo ndiyo ya karibuni zaidi miongoni mwa mkururo wa makubaliano yaliyofikiwa hayatakuwa yametekelezwa, basi baraza hilo la usalama litamuwekea vikwazo waziri wa ulinzi wa Sudan Kusini pamoja na maafisa wengine watano na pia uwezekano wa kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kuuziwa silaha.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Halley
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki HalleyPicha: picture-alliance/ZumaPress/M. Brochstein

Nikki Haley: Marekani yapoteza subira

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ameliambia baraza hilo kuwa Marekani imepoteza subira.

"Marekani imepoteza subira yake. Hali iliyoko kwa sasa haikubaliki. Wakati umewadia wa sisi sote kudai hali nzuri kwa raia wa Sudan Kusini"

Ethiopia na Guinea ya Ekweta zilikosa kupiga kura huku zikisema ni sharti juhudi za amani zipewe muda zaidi, lakini Cote Di'Voire, ambayo ni nchi ya tatu ya Afrika katika baraza hilo iliunga mkono azimio hilo.

Marekani imeorodhesha majina ya maafisa sita, lakini uamuzi wa mwisho wa kuwawekea vikwazo vya usafiri na kutaifishwa kwa mali zao, utatolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa Akuel Bona amesema azimio la kuwawekea maafisa wa nchi yake vikwazo si sawa na huenda lisizae matunda yanayotarajiwa.

"Mchakato wa amani wa Sudan Kusini kwa sasa umefikia hatua muhimu. Kuna matumaini na nyongeza iliyoambatanishwa kwa azimio hili inasikitisha, na wala haisaidii kitu. Hatari iliyoko ni kuwa huenda hilo lisifanikishe kile kinachotarajiwa na wale waliounga mkono azimio hilo"

Wanajeshi wa Sudan Kusini wakishika doria mjini Malakal Oktoba 2016
Wanajeshi wa Sudan Kusini wakishika doria mjini Malakal Oktoba 2016Picha: picture-alliance/Photoshot/G. Julius

Mawaziri walengwa kuwekewa vikwazo

Baadhi ya maafisa wanaolengwa kuwekewa vikwazo ni pamoja na waziri wa ulinzi Kuol Manyang Juuk kwa kuongoza mashambulizi kaskazini mashariki mwa mji wa Pagak ambao ulikamatwa na waasi mwaka 2017.

Wengine ni kaimu waziri wa mambo ya nchi za nje, Martina Elia Lomuro kwa kutishia vyombo vya habari, kuzuia misaada ya kiutu na kuhujumu kazi ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini. 

Waziri wa habari Michael Makuel ametajwa kwa madai ya kuhusika katika kupanga shambulizi katika kambi ya Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2014.

Balozi wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa, Tekeda Alemu ameonya kuwa hatua ya kuweka vikwazo inaweza kupelekea kuvunjika kwa juhudi za amani za kanda hiyo zinazoongozwa na jumuiya ya ushirikiano wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika- IGAD

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga