1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kusaidia kulinda mipaka ya Libya

Elizabeth Shoo31 Januari 2013

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya wameanzisha mipango ya kuulinda mpaka wa Libya. Eneo hilo la mpaka lenye urefu wa maelfu ya kilometa limewapa mwanya watu wanaovusha silaha kimagendo.

https://p.dw.com/p/17VOu
GettyImages 160414414 Slovenia Foreign Affairs minister Karl Erjavec and EU commissioner for International Cooperation, Humanitarian Aid and Crisis Response Kristalina Georgieva and High Representative of the European Union for Foreign Affairs and Security Policy Catherine Ashton (LtR) talk prior to a Foreign Affairs Council on January 31, 2013 at the EU Headquarters in Brussels. The Council will discuss the situation in the EU's southern neighbourhood, in particular in Syria and Egypt, and will prepare the forthcoming European Council debate on the Arab Spring. Ministers will also discuss the priorities of the foreign policy of the new US administration.They will be informed of the situation in Mali and the action taken by the EU in response to the special session of the last Foreign Affairs Council devoted to Mali. AFP PHOTO GEORGES GOBET (Photo credit should read GEORGES GOBET/AFP/Getty Images)
Außenministertreffen in BrüsselPicha: AFP/Getty Images

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Bi Catherine Ashton, ameeleza kwamba hatua ya kuongeza uwezo wa Libya kulinda mipaka yake ni ya muhimu, si kwa nchi hiyo tu bali kwa eneo zima. Tangu kuangushwa madarakani kwa Muamar Gaddafi mwaka 2011, Libya imekumbwa na changamoto kulinda mipaka yake yenye ulinzi finyu. Wataalamu wanaamini kwamba silaha kutoka Libya zimekuwa zikivushwa na kupelekwa katika nchi jirani kama Mali, ambapo zinatumika kwenye mapigano.

Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wameeleza kwamba utawala wa Libya umeshindwa kudhibiti hasa mpaka wake wa kusini unaoitenga nchi hiyo na Algeria, Niger, Chad na Sudan. Inaelezwa kwamba watu wenye kubeba silaha nzito nzito huuvuka mpaka wa Libya na kupitisha silaha na madawa ya kulevya kimagendo. Wataalamu wa Umoja wa Ulaya wamelenga kutoa mafunzo kwa maafisa wa usalama wanaolinda mipaka ya Libya ili kuimarisha usalama. Wataalamu hao watapelekwa Libya kwa kipindi cha miaka miwili kwanza na baadaye muda wao unaweza kuongezwa kwa mwaka mmoja.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza David CameronPicha: Reuters

Uingereza yaahidi kuisaidia Libya

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amefanya ziara ya kushtukiza katika mji mkuu wa Libya, Tripoli. Ziara ya Cameron inakuja siku chache tu baada ya Uingereza kutoa angalizo juu ya tishio la mashambulizi kwa ubalozi wa nchi yake uliopo Tripoli. Ofisi ya waziri mkuu huyo ilitoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, inayoeleza kwamba Cameron anakwenda Libya kujadili namna ambavyo Uingereza inaweza kusaidia katika kujenga Libya yenye nguvu, ustawi na demokrasia.

Baada ya kuwasili, Cameron na waziri wa mambo ya ndani wa Libya Ashur Shwayel walikitembelea chuo kimoja cha polisi ambapo ilifanyika hafla ya kuwapandisha cheo maofisa wa polisi. Cameron yuko njiani kuelekea Liberia ambapo atahudhuria mkutano wa kiamataifa kuhusu maendeleo.

Wanajeshi wa Ufaransa wanapambana na waasi Mali
Wanajeshi wa Ufaransa wanapambana na waasi MaliPicha: dapd

Katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, ilizungumziwa pia hali nchini Mali. Mawaziri hao wamewataka wanajeshi wa nchi za Afrika kuchukua nafasi ya wanajeshi wa Ufaransa haraka iwezekanavyo. Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji, Didier Reynerds, amesema kwamba anatarajia kuwa operesheni inayoendelea Mali itakuwa ya kimataifa na itakayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na majeshi ya nchi za Kiafrika.

Nchini Mali kwenyewe msemaji mmoja wa jeshi ameeleza kwamba bomu la kutegwa ardhini limewaua wanajeshi wanne na kujeruhi wengine watano baada ya gari walilokuwa wakisafiria kufyatua bomu hilo.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef