1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu bilioni 2 duniani hawapati maji salama

22 Machi 2024

Umoja wa Mataifa umesema hii leo kuwa ushirikiano baina ya mataifa jirani kuhusu rasilimali za pamoja za maji unaweza kusaidia kuepusha mizzozo na kujenga amani, na kuyahimiza mataifa kujiunga na mkataba wake wa maji.

https://p.dw.com/p/4e0gI
Utekaji maji- Somaliland
Wanawake wakichota maji kutoka jamii ya Xidhinta huko SomalilandPicha: Daniel Jukes/AP Photo/picture alliance

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na Utamadini-UNESCO limebainisha kuwa watu bilioni 2.2 duniani hawapati maji salama ya kunywa, huku wengine bilioni 3.5 wakikosa hudumu zinazosimamiwa kwa usalama za usafi. UNICEF: Watoto 1,000 hufa kila siku kwa kunywa maji machafu

Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa uhaba wa maji kote duniani, ushirikiano wa kuvuka mipaka kuhusu suala la maji unazidi kuwa muhimu kwa utulivu wa kikanda na uzuwiaji wa mizozo. Katibu wa Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa Sonja Koeppel, amesema maji na amani vinahusiana kwa karibu sana.

Afghanistan-Uhaba wa maji
Watoto katika jimbo la Balkh huko Afghanistan wakiwa wamebeba madumu ya majiPicha: Rahmat Alizadah/Xinhua/imago

Amebainisha kuwa zaidi ya silimia 60 ya vyanzo vyote vya maji salama vinashirikisha mataifa mawili au zaidi, ikiwemo mito mikubwa kama vile Rhine na Danube ya barani Ulaya, Mto Mekong barani Asia, Mto Nile barani Afrika na Amazoni katika Kanda ya Amerika Kusini. Amesema ushirikiano juu ya rasilmali maji ni muhimu kwa amani, na maendeleo ya hatua za kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Upatikanaji wa Maji Safi na Salama

Amesema maji ni rasilimali muhimu kiasi kwamba yana nguvu ya kuzileta nchi zilizoko kwenye mzozo katika meza ya mazungumzo, na kufungua mlango wa ushirikiano katika maeneo mengine pia. India na Pakistan kwa mfano zina makubaliano ya ushirikiano kuhusu matumizi ya Mto Indus. Na makubaliano yaliofikiwa kati ya Senegal, Mauritania, Guinea na Gambia katika miaka ya 1970 kuhusu bonde la Mto Senegal yameziwezesha kufadhili kwa pamoja na kujenga miundombinu inayosambaza maji kwa mataifa yote manne.

Hata wakati mivutano ya kisiasa inapotawala kati ya mataifa, Koeppel anasema ushirikiano huu wa rasilimali maji umeendelea kuwepo. Jumla ya mataifa 153 yanashiriki rasilimali za maji kote duniani, lakini ni 24 tu kati ya hayo yaliosaini makubaliano mbalimbali kuhusu maji yao ya pamoja, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika taarifa yake ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Maji leo Ijumaa.Changamoto ya upatikanaji maji salama

Guterres amehimiza kuongeza juhudi za ushirikiano wa kuvuka mipaka, na kuyarai mataifa kujiunga na kutekeleza mkataba wa maji wa Umoja wa Mataifa, akisema hatua kwa ajili ya maji ni hatua kwa ajili ya amani. Mkataba huo ulianzishwa mwaka 1992 kusaidia kukuza usimamizi wa pamoja wa uwajibikaji wa rasilimali maji katika kanda ya Ulaya, lakini ulitanuliwa mwaka 2016 kuyajumlisha mataifa kote duniani, na sasa una mataifa 52 wanachama, hasa kutoka  Ulaya, Asia na Afrika.

Burkina Faso
Wakimbizi kutoka Kaskazini mwa Burkina Faso wakikinga maji Picha: OLYMPIA DE MAISMONT/AFP/Getty Images

Soma: Ni kiasi gani cha maji unachohitaji mwili wetu?

Wakati miito hiyo ya ushirikiano wa mataifa kuhusu rasilimali ya maji ukitolewa, shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNICEF, limesema watu bilioni 2.2 duniani hawapati maji salaama ya kunywa, na wengine bilioni 3.5 wanakosa huduma salama za usafi.

Mkurungezi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay, amesema mtu mmoja kati ya wawili kote duniani aliteseka kutokana na uhaba wa maji kwa miezi kadhaa ya mwaka, na kuongeza kuwa katika baadhi ya maeneo ya dunia, uhaba wa maji umegeuka kuwa kanuni kuliko kuwa jambo la kipekee.