1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yawahimiza viongozi Somalia kuafikiana juu ya uchaguzi

Amina Mjahid
10 Februari 2021

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitolea mwito serikali kuu ya Somalia na tawala majimbo kurejea haraka katika mazungumzo na kukubaliana juu ya utaratibu wa kuandaa uchaguzi mkuu haraka iwezekanavyo.

https://p.dw.com/p/3p9bS
Somalia Mogadischu Parlament
Picha: Sadak Mohamed/AA/picture alliance

Makubaiano yaliofikiwa mwezi Septemba mwaka jana yanampa rais Mohamed Abdullahi Mohamed na viongozi wengine serikalini nafasi ya kubakia madarakani iwapo italazimika baada ya tarehe 8 iliyopangwa kuwa siku ya uchaguzi wa Somalia, lakini mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Somalia James Swan, ametahadharisha kuwa hatua hiyo ya kuendelea kubakia madarakani inaweza kusababisha mgogoro wa kisiasa.

Baada ya mkutano wa faragha uliofanywa na James Swan, wanachama wa Baraza hilo la Umoja wa Mataifa walitoa taarifa wakiridhia na kukaribisha juhudi zinazifanywa na viongozi wa serikali ya shirikisho na majimbo nchini Somalia, kutafuta muafaka wa kutekeleza makubaliano ya mwezi Septemba na pia kuonyesha wasiwasi wao kuhusu mazungumzo ya Jumamosi yaliomalizika bila kufikiwa muafaka.

soma zaidi: Upinzani Somalia watangaza kutomtambua rais

Taarifa hiyo iliwataka viongozi wa serikali kurejea katika meza ya mazungumzo haraka, na kufanya kazi pamoja kwaajili ya manufaa ya wanachi wa Somalia huku ikitoa wito wa kufanyika mipango ya kuandaa uchaguzi haraka utakaowajumuisha watu wote. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika tarahe 15 mwezi wa Februari.

Wakati hayo yakiarifiwa Balozi wa Estonia katika Umoja wa Mataifa Sven Jurgenson, ameyaunga mkono mazungumzo yajayo akisema wanasiasa wa Somalia ni lazima waweke kando tofauti zao na kufanya maamuzi kwa kuzingatia masilahi ya nchi na watu wake.

Rais Mohammed Abdullahi asema bado kuna matumaini ya kuelewana

Russland Sochi | Präsident Somalia | Mohamed Abdullahi Mohamed
Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Picha: Vladimir Smirnov/Imago Images

Kwa upande wake rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed, anayewania muhula wake wa pili wa miaka minne madarakani, ameyalaumu mataifa ya kigeni ambayo hakuyataja kwa kufelisha mazungumzo na kuyalaumu majimbo ya Puntland na Jubbaland kukataa kuunga mkono makubaliano yaliotiwa saini mwezi Septemba.

Licha ya hayo rais Mohamed Abdullahi amesema bado kuna matumaini ya kusonga mbele, akisema kinachohitajika ni muda wa kuzungumza na kusuluhisha matatizo yanayowakabili.

Hatua ya kucheleweshwa kwa uchaguzi nchini Somalia inalipa nafasi zaidi  ya kujipanga kundi la wanamgambo la Al Shabaab lililoapa kushambulia wakati wa uchaguzi. Wiki iliyopita kundi hilo lilitoa mkanda wa video unaomkashifu rais pamoja na mchakato mzima wa uchaguzi likisema umezungukwa na ufisadi.

soma zaidi: Somalia: Watu watano wauawa kwenye shambulio la kujitoa mhanga

Kando na hayo Somalia bado inajipanga upya baada ya wanajeshi takriban 700 wa Marekani kuondoka nchini Somalia katikati ya mwezi Januari na huenda ikakumbana na changamoto zaidi ya kiusalama baada ya maafisa 20,000 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2021.

Taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesifia jukumu la Umoja wa Afrika la kushinikiza mazungumzmo kati ya makundi hasimu nchini Somalia, na pia imelaani mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na kundi la Al-Shabab na kuihakikishia somalia kuwa itaiunga mkono ili kufikia uhuru wa kisiasa.

Chanzo: ap