1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGabon

Upinzani Gabon washinikiza wanajeshi kukabidhi madaraka

Sylvia Mwehozi
1 Septemba 2023

Muungano wa vyama vya upinzani wa Gabon, umetoa mwito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhimiza viongozi waliompindua Rais Ali Bongo, kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

https://p.dw.com/p/4Vr9N
Gabun | Militärputsch
Picha: AA/picture alliance

Msemaji wa muungano huo unaojulikana kama Alternance 2023, Alexandra Pangha, amelieleza shirika la habari la BBC kwamba wamefurahi Bongo kupinduliwa, lakini wana matumaini kwamba viongozi wa mapinduzi watakabidhi mamlaka kwa utawala wa kiraia. Muungano huo unashinikiza kuhesabiwa upya kwa kura katika uchaguzi wa Jumanne, ukikariri ushindi wa mgombea wa upinzani Albert Ondo Ossa.

Naye mkurugenzi wa kampeni wa mgombea wa upinzani Mike Jocktane amesema kuwa wako tayari kujadiliana na viongozi wa kijeshi kuhusu kipindi cha mpito.

Soma pia: Mataifa ya Afrika ya Kati yachukulia vipi mapinduzi Gabon ?

"Vuguvugu la Alternance 2023 unawaalika wawakilishi wa vikosi vya ulinzi na usalama kujadili hali katika mfumo wa kizalendo na uwajibikaji, na kutafuta suluhisho bora kati ya watu wa Gabon ili kuwezesha nchi yetu kujikwamua kutoka katika hali hii tukiwa imara zaidi kuliko hapo awali."

Kiongozi wa mapinduzi Brice Oligui Nguema anatarajiwa kuapishwa siku ya Jumatatu kama rais wa mpito.