1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani utapinga kisheria kuhesabiwa tena kwa kura Zimbabwe

Kalyango Siraj14 Aprili 2008

Mahakama kuu kuamua kuhusu kutangazwa kwa matokeo

https://p.dw.com/p/DhPe
Viongozi wa mataifa ya jumuia ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC nje ya ukumbi wa mikutano wa Mulungushi Lusaka jumapili 14 Machi 2008 baada ya mkutano wa dharura uliojadilia hali ya kisiasa nchini ZimbabwePicha: AP

Shinikizo la kikanda limeongezeka kwa Zimbabwe baada ya mkutano mkuu wa viongozi wa nchi za kanda ya Kusini mwa Afrika kutaka matokeo ya uchaguzi kutolewa haraka.Mkutano huo uliofanyika Zambia ulikuwa na nia ya kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe.

Na katika matukio mengine upande wa upinzani unasema utapinga mahakamani uamuzi wa tume ya uchaguzi kuhesabiwa tena kura za ubunge za uchaguzi uliofanyika mwezi jana.

Mahakama kuu ya Zimbabwe inatarajiwa leo jumatatu kutoa kauli muhimu kuhusu matokeo urais ya uchaguzi uliofanyika siku 16 zilizopita.

Uamuzi wa leo jumatatu wa mahakama unaweza ukamaliza kipindi kirefu cha kusubiri kujua nani kati ya rais Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgen Tsvangirai alieshinda.

Chama cha Movement for Democratic Change-MDC ambacho kinadia kuwa kiongozi wake Tsvangirai alimbwaga Mugabe katika uchaguzi mkuu wa Machi 29,kinaitaka mahakama hiyo ishurutishe tume ya uchaguzi inayodhibitiwa na serikali itangaze matokeo.

Kushindwa kwa tume ya uchaguzi kutoa matangazo kumezusha mshangao ndani na nje ya Zimbabwe.Mkutano wa kilele wa jumuia ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC ulimalizika jana mjini Lusaka Zambia kwa mwito,kupitia katibu wake mkuu Thomas Salomao, kwa tume ya uchaguzi kutoa matokeo haraka.

Chama tawala cha ZANU PF kinasema kuwa hakuna kati ya viongozi hao wawili,Mugabe au Tsvangirai,aliepata kura za kutosha,na hivyo kuhitajika duru ya pili.

Aidha chama hicho kinataka matokeo ya uchaguzi wa baadhi ya majimbo yahesabiwe tena.Vyombo vya habari nchini Zimbabwe vinasema kuwa matokeo kutoka majimbo 23 yatahesabiwa tena.

Mabadiliko yoyote katika matokeo ya ubunge ya viti tisa tu utakipa chama cha rais Mugabe cha ZANU PF wingi wa viti bungeni,kilichoupoteza katika uchaguzi wa juzi.

Wiki mbili zimekatika na matokeo ya urais baado hayajatolewa.

Chama cha upinzani cha MDC kinamlaumu rais Mugabe kwa kukataa kutolewa kwa matokeo akiwa na nia ya kubadili matokeo.

Lakini macho yote yamemulikwa kwa hakimu Tendai Uchena atakapo toa uamuzi ikiwa kuishinikiza tume ya uchaguzi itoe matangazo haraka.

Kwa mda huohuo waandishi habari wawili wakigeni waliokamatwa juzi kwa madai ya kuripoti kuhusu uchaguzi wa Zimbabwe bila ya kibali maalum,watafikishwa mbele ya mahakamani baadae leo jumatatu mjini Harare.