Uruguay na Uholanzi kupambana katika nusu fainali ya kwanza kombe la dunia
6 Julai 2010Saa na dakika zinaendelea kuyoyoma kuelekea nusu fainali ya kwanza ya kombe la dunia mwaka huu 2010 nchini Afrika kusini. Uruguay na Uholanzi zinakaribia kuingia dimbani kuamua nani ataingia katika fainali ya mwaka huu ya kombe la dunia.
Uruguay haipewi nafasi kubwa mbele ya Uholanzi leo kuingia katika fainali baada ya kuiondoa Ghana katika mchezo wa robo fainali uliozusha maswali kadha, lakini Ghana ilipokelewa kama mashujaa waliporejea nyumbani, na kila mpenda soka katika bara la Afrika aliridhika kuona kuwa Ghana haikutolewa kama timu nyingine za bara hilo.
Uruguay, ambayo imo katika nusu fainali yake ya kwanza katika muda wa miaka 40 iliyopita, inaangalia miaka yake ya nyuma ambapo ilipata mafanikio wakati waliponyakua kombe hilo katika mwaka 1930 na 1950.
Wadachi, Uholanzi, timu timu bora ambayo haijawahi kushinda kombe la dunia licha ya aina ya mchezo wao wa wazi ambao ni maarufu duniani kote , hii leo ndio wanaopewa nafasi ya juu kuweza kuibuka na ushindi, wakiongozwa na wachezaji hatari wa kiungo Arjen Robben, Wesley Sneijder na Dirk Kuyt.
Uruguay huenda ikawakosa wachezaji wake watatu muhimu, na mzigo mkubwa utamuangukia mshambuliaji nyota Diego Forlan, ambaye alipachika bao la kusawazisha dhidi ya Ghana katika robo fainali.
Kocha wa Uholanzi Bert van Marwijk amesisitiza kuwa timu yake haitaonyesha ishara zozote za dharau kama ilivyofanya siku za nyuma.
Huu ni wakati ambao nimeuzungumzia miaka miwili iliyopita, kwamba iwapo tunashinda dhidi ya timu kama Brazil na tuko juu ya dunia, na kisha unakuwa na mchezo mwingine, na mchezo huo ni dhidi ya Uruguay, hawa ni wapiganaji, si rahisi kusalim amri , na kwa hiyo inatubidi kuwa makini sana.
Wakati vikosi hivyo viwili vinaota ndoto ya mafanikio, Black Star wa Ghana walikuwa wakielea katika wimbi la mapenzi makubwa ya taifa lao ambapo walilakiwa kama mashujaa licha ya kutolewa katika kinyang'anyiro hicho kwa hali ya kusikitisha dhidi ya Uruguay.
Maelfu ya watu walifika katika uwanja wa ndege kuwalaki, Black Stars jana Jumatatu wakiimiminia maji ndege iliyowachukua na kuwapokea kwa heshima ya zulia jekundu. Kundi kubwa la watu lilifurika katika uwanja huo wa ndege mjini Accra wakipuliza matarumbeta ya vuvuzela, wakiimba na kupiga ngoma.
Ghana ilikuwa timu pekee kutoka idadi ya timu sita katika bara la Afrika ambayo imefikia hatua ya robo fainali, na kujiunga na timu nyingine mbili za bara la Afrika ambazo zimeweza kufikia hatua hiyo, Cameroon mwaka 1990 na Senegal mwaka 2002.
Wakati huo huo shirikisho la soka duniani FIFA linasaka hoteli ya kuiweka timu ya Uholanzi baada ya maafisa wa timu hiyo kushindwa kujiwekea vyumba hadi mwisho wa mashindano hayo. Shirikisho la soka la Uholanzi liliomba kubaki katika hoteli waliyoko hivi sasa mjini Johannesburg ya Sandton Hilton hadi Julai 5 na hoteli hiyo sasa imejaa.
Wakati shirikisho la FIFA huziweka timu zote usiku mmoja kabla na baada ya mchezo, timu hulazimika kufanya utaratibu wao kwa ajili ya siku nyinginezo. Shirikisho la kandanda la Uholanzi limethibitisha kuwa timu yao inapaswa kuondoka katika hoteli hiyo kwa kuwa imekwisha jaa kwa kipindi chote cha mashindano hayo.
Nahodha wa zamani wa Uholanzi Ruud Gullit amesisitiza kuwa mchezaji wa pembeni Arjen Robben atakuwa muhimu katika kuishinda Uruguay katika mchezo wao wa nusu fainali hii leo. Gullit ni nahodha pekee wa Uholanzi ambaye ameweza kubeba kombe katika mashindano makubwa akiwa na timu ya taifa ya Uholanzi baada ya kushinda ubingwa wa bara la Ulaya mwaka 1988.
Ameongeza kuwa kikosi cha kocha Bert van Marwijk kinaweza kuondoa machungu ya kufungwa mara kwa mara katika fainali, kama ilivyotokea mwaka 1974 na 1978 katika kombe la dunia.
Mwandishi: Sekione Kitojo/RTRE/AFPE
Mwandishi: Abdul-Rahman