1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yataka vikwazo ili kumaliza vita Sudan Kusini

Admin.WagnerD17 Septemba 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemwalika Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuhudhuria mkutano wa viongozi wa dunia utakaofanyika mnamo mwezi huu,kwenye Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/1GXhw
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Urusi imesema inapinga vikwazo vipya vilivyopendekezwa na Marekani dhidi ya mkuu wa majeshi ya Sudan Kusini na dhidi ya Jenerali wa zamani ambae sasa ni kamanda mwasi.

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin ameeleza kwamba mawaziri wa mambo ya nje wa Sudan na Sudan Kusini waliokutana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi mjini Moscow hivi karibuni walitia saini tamko la pamoja kupinga vikwazo kuhusiana na mgogoro wa Sudan Kusini.

Balozi Churkin aliwaambia waandishi wa habari kwamba tamko hilo linapaswa kutiliwa maanani. Balozi huyo ameishutumu Marekani kwa kulitumia neno vikwazo wakati wote.Amesema aghalabu vikwazo vinasababisha madhara zaidi.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Sudan na Sudan Kusini wameazimia kuyazingatia makubaliano yote juu ya kudumisha amani,baada ya mkutano wao wa mjini Moscow.

Angola pia yapinga vikwazo

Na habari zaidi zinasema Angola imeungana na Urusi katika kuvipinga vikwazo dhidi ya majenerali hao wawili wa Sudan Kusini, vilivyopendekezwa na Marekani.

Vikwazo hivyo dhidi Jenerali Paul Malong na jenerali wa zamani Johnson Olony ni pamoja na kuwanyima vibali vya kusafiria na kuzizuia mali zao.

Mapigano yalizuka katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Sudan Kusini miaka miwili iliyopita baada ya Rais Salva Kirr kudai kwamba Makamu wake Riek Machar alikuwa anapanga njama za kuiangusha serikali yake. Hatua ya Rais Kiir ya kumfukuza makamu wake ilisababisha mapigano ya kikabila.

Na licha ya kutia saini mkataba wa kusimamisha mapigano mnamo mwezi wa Agosti, mapambano yameendelea.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemwalika Rais Salva Kiir na Riek Machar kuhudhuria mkutano wa ngazi ya juu utakaoujadili mgogoro wa Sudan Kusini tarehe 29 wakati wa Baraza Kuu la Umoja wa mataifa, litakalohudhuriwa na viongozi wa dunia

Mwandishi:Mtullya Abdu. ape/

Mhariri: Gakuba Daniel