1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yalishupalia kundi la IS

Admin.WagnerD30 Juni 2016

Uturuki imewakamata watu 13 kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi kwenye uwanja wa ndege wa Istanbul. Nchi hiyo imesema imewatambua washambuliaji wote watatu kuwa raia wa kigeni, kutoka Urusi, Uzbekstan na Kyrgyzstan.

https://p.dw.com/p/1JGs5
Usalama umeimarishwa Uturuki baada ya shambulizi ya Istanbul
Usalama umeimarishwa Uturuki baada ya shambulizi ya IstanbulPicha: picture-alliance/AA/A. Hudaverdi Yaman

Haya yanajiri wakati idadi ya watu waliopoteza maisha katika shambulizi kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Istanbul Jumanne usiku kupanda hadi watu 43, miongoni mwao 19 wakiwa raia wa kigeni. Wengine wapatao 200 walijeruhiwa katika shambulio hilo baya.

Polisi wa Uturuki wamefanya misako mikali katika vitongoji vya Istanbul asubuhi ya leo, na kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Efkan Ala, washukiwa 13 wametiwa mbaroni. Hili lilikuwa shambulio baya zaidi katika mfululizo wa mengine mengi yaliyoilenga Uturuki, yakidaiwa kufanywa ama na wanamgambo wa kikurdi, au wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Hili la Istanbul limefanywa mwanzoni mwa msimu muhimu wa utalii, wa majira ya kiangazi.

IS yashukiwa

Ingawa waziri Ala amesema bado hawajawa na uhakika kamili kuhusu kundi lililoyafanya mashambulizi hayo, dalili za mwanzo zinaashiria mkono wa IS, madai ambayo yameungwa mkono na mkurugenzi mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani,CIA, John Brennan.

Watu 43 wameuawa katika shambulizi la kigaidi kwenye uwanja wa ndege wa Istanbul
Watu 43 wameuawa katika shambulizi la kigaidi kwenye uwanja wa ndege wa IstanbulPicha: DW/T. Stevenson

Taarifa kamili zimeanza kupatikana kuhusu shambulio la Jumanne usiku mjini Istanbul, zikisema washambuliaji waliingia uwanjani hapo wakisafiri kwa taxi, na kisha wakaanza kuwamiminia watu risasi na kujitoa mhanga kwa kuripua mabomu yao.

Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim amesema magaidi hao walishindwa kupita katika kituo cha ukaguzi uwanjani Istanbul, ndipo wakarudi nyuma na kurejea na bunduki za masafa marefu zilizokuwa katika masanduku yao, wakapita katika sehemu ya ukaguzi wakifyatua risasi kiholela, na kisha mmoja alijiripua.

Juhudi mpya kuhakikisha usalama viwanjani

Waziri mkuu huyo alisema huenda zikahitajika juhudi zaidi katika katika kuhakikisha usalama viwanjani.

Binali Yildirim, Waziri Mkuu wa Uturuki
Binali Yildirim, Waziri Mkuu wa UturukiPicha: Reuters/U. Bektas

''Mashambulizi haya yamedhihirisha kwamba ukaguzi wa viwanjani kutumia mionzi hautoshi. Tunapaswa kuwa tayari kwa mashambulizi mengine ya bunduki kutokea nje ya uwanja. Pengine tunahitaji kujihadhari zaidi''. Amesema Waziri Mkuu Yildirim.

Hata hivyo sheria za Uturuki za kupambana na ugaidi zimekosolewa na Umoja wa Ulaya, ambao Uturuki inataka kuwa mwanachama wake. Umoja wa Ulaya unasema sheria hizo zinatumiwa kukandamiza uhuru wa kutoa mawazo, na kutaka zirekebishwe.

Umoja wa Ulaya umeyafungamanisha marekebisho hayo na masharti inayotakiwa kuyatekeleza Uturuki, ili raia wake waruhusiwe kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya bila viza.

Uturuki inayakataa madai hayo ya Umoja wa Ulaya, ikisema mashariti ya umoja huo yanawapa nguvu magaidi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo