1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Amerika Kusini kukutana leo nchini Trinidad na Tobago

Charo Josephat17 Aprili 2009

Swala la Cuba linatarajiwa kuugubika mkutano huo

https://p.dw.com/p/HYox
Rais Wa Cuba Raul CastroPicha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama na viongozi wa Amerika Kusini wanajiandaa kuwa na majadiliano makali kuhusu hali ya baadaye ya Cuba kwenye mkutano wa nchi za Amerika Kusini unaoanza leo nchini Trinidad na Tobago. Rais Obama anahudhuria mkutano huo akitokea Mexico ambako ameahidi kuisaidia nchi hiyo kupambana na magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Rais Obama na mshirika mkubwa wa Cuba, rais wa Venezuela Hugo Chavez wamedhihirisha misimamo inayopingana siku moja kabla mkutano wa nchi za Amerika Kusini kuanza hii leo nchini Trinidad na Tobago. Swala la Cuba linatarajiwa kupewa kipaumbele na kuugubika mkutano huo.

Rais Obama, akiwa nchini Mexico amesema uhusiano kati ya Marekani na Cuba ambao umekuwa katika mkwamo kwa miaka 50 hautabadilika na kuboreka katika siku moja. Hata hivyo amesitiza kuwa hatua yake ya kuondoa vikwazo vya usafiri na utumaji wa fedha nchini Cuba ni ishara kwamba Marekani inataka kubadili uhusiano wake na kisiwa hivho. Ingawa kikwazo cha kiuchumi cha miaka 47 dhidi ya Cuba bado kinabakia, rais Obama anasema sasa ni wakati wa Cuba kudhihirisha inataka kufanya mageuzi.

"Cuba inatakiwa kutoa ishara kwamba itafanya mageuzi kuhusu jinsi nchi hiyo inavyoendeshwa yatakayohakikisha wafungwa wa kisiasa wanaachiwa huru, watu waweze kutoa maoni yao kwa uhuru, waweze kusafiri, kuandika barua, kwenda kanisani na kufanya mambo ambayo watu wengine kote ulimwenguni wanaweza kufanya."

Rais wa Cuba Raul Castro amesisitiza kwamba utawala wake uko tayari kujadiliana na Marekani kuhusu haki za binadamu, uhuru wa vyombo vya habari, wafungwa wa kisiasa na kila kitu inachotaka kukijadili kwa sharti kwamba ichukuliwe kuwa taifa sawa na Marekani.

Kiongozi huyo amepuuza wito wa waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Hilary Clinton, kutaka wafungwa wote wa kisiasa waachiwe huru na kusema utawala wake hauna nia ya kuwa tena mwanachama wa muungano wa nchi za bara la Amerika, tangu ilipofukuzwa mnamo mwaka 1962 kufuatia ombi la Marekani.

Venezuela Präsident Hugo Chavez mit tocher in Caracas vor Sendung Alo Presidente
Rais wa Venezuela Hugo Chavez na mtoto wake wa kike Maria ChavezPicha: AP

Chavez kutumia turufu

Rais Hugo Chavez wa Venezuela alikutana jana na rais wa Cuba Raul Castro na washirika wengine wa mrengo wa kushoto kutoka Bolivia, Honduras, Nicaragua na Paraguay kwenye kongamano dogo la kikanda nchini Venezuela la kuupinga mkutano wa Trinidad na Tobago. Chavez ameashiria kulizusha na kulipa kipaumbele swala la Cuba kwenye mkutano huo wa nchi za Amerika Kusini.

Kiongozi huyo pia amesema atatumia kura yake ya turufu kupinga taarifa itakayotolewa baada ya mkutano huo kumalizika kwa sababu hailaani kutoshirikishwa kwa Cuba kwenye mkutano huo. Rais Obama hana mpango wa kukutana na rais Chavez katika mkutano huo.

Dawa za kulevya Mexico

Rais Obama anahudhuria mkutano wa Trinidad na Tobago akitokea Mexico ambako ameahidi kuisaidia nchi hiyo kupambana na magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Amesema Marekani ina jukumu la kufanya katika vita hivyo na kuahidi kushirikiana kikamilifu na Mexico.

"Tumejitolea kikamilifu kushirikiana na Mexico kuhakikisha tunakabiliana na tatizo hili katika pande zote mbili za mpaka"

Obama und Calderon in Mexico
Rais wa Marekani Barack Obama (kushoto) na rais wa Mexico Felipe CalderonPicha: AP

Rais Obama ameipongeza Mexico kwa ufanisi uliopatikana katika vita dhidi ya dawa za kulevya lakini akasema Marekani inabeba dhamana kwa tatizo hilo. Amesema mahitaji ya dawa za kulevya nchini Marekani inayasaidia magenge ya ulanguzi wa dawahizo kuendelea kufanya biashara.

Mwandishi:Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Saumu Mwasimba