1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia wamtakia afueni Trump

Lilian Mtono
2 Oktoba 2020

Rais wa Marekani Donald Trump amesema yeye na mkewe Melania wameambukizwa virusi vya corona na wanakwenda kukaa karantini, ikiwa ni mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi wa urais utakaofanyika Novemba 3 mwaka huu. 

https://p.dw.com/p/3jKKu
USA Cleveland Donald Trump und Melania
Picha: Carlos Barria/Reuters

Hata hivyo daktari wa Trump, Sean Conley amesema hali yake ni nzuri na bado anaweza kuendelea na majukumu yake akiwa karantini na kusema watasalia ikulu kwa muda wote wa karantini. Trump mwenye miaka 74 mara ya kwanza alitangaza kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba yeye na mkewe Melania wameambukizwa.

Athari ya awali kabisa baada tu ya taarifa hii ni kuahirishwa kwa mkutano wa kampeni wa Trump uliotarajiwa kufanyika baadae leo huko Florida.

Ni Alhamisi hii tu Trump alisema kwenye hotuba yake akiwa New York kwamba janga hilo la corona limedhibitiwa na mwaka ujao utakuwa mwaka wa mambo makubwa kuwahi kushuhudiwa kwenye historia ya Marekani.

Lakini sasa kiongozi huyo ambaye mara kwa mara alielezea mashaka yake kuhusiana na ukubwa wa virusi hivyo, licha ya zaidi ya watu 200,000 kufariki dunia nchini humo, ndiye sasa anakuwa kiongozi wa juu kabisa ulimwenguni kuugua maradhi ya COVID 19 hali inayothibitisha kwamba pamoja na rasilimali zote za ikulu ya White House, lakini hazikuweza kumzuia kuambukizwa.

Taarifa ya kuambukizwa kwake inafuatia ile ya msaidizi wake wa karibu kabisa, Hope Hicks aliyetangazwa kuambukizwa siku ya Alhamisi. Hicks alisafiri na Trump kwenda Cleveland kwenye mdahalo wake wa kwanza na Biden siku ya Jumanne na Jumatano aliambatana naye kwenye kampeni za Minnesota.

Hope Hicks Beraterin von US-Präsident Trump
Hope Hicks, msaidizi wa karibu kabisa wa rais Trump aliyeambukizwa virusi vya corona kabla ya kutolewa taarifa za kuambuzwa Trump.Picha: Leah Millis/Reuters

Hata hivyo, licha ya taarifa za kuambukizwa Hicks, Trump alisafiri naye tena kwenye ndege ya rais ya Air Force One siku ya Alhamisi kukutana na wafadhili huko New Jersey.

Mgombea wa urais kutoka chama cha Democratic, Joe Biden ambaye amekuwa akitumia ukosoaji wa namna chama cha Republican kinavyokabiliana na janga hilo kama ajenda kuu kwenye kampeni zake hakutoa tamko lolote mara moja kuhusiana na hali ya kiafya ya rais Trump baada ya taarifa hiyo.

Kisayansi, uzito mkubwa na umri wa Trump ni sababu tosha zinazomuweka katika hatari kubwa kama ilivyo mtu yeyote anayepata maambukizi ya virusi hivyo.

EU-Sondergipfel | Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekuwa mmoja wa viongozi waliomtakia heri na uponyaji rais TrumpPicha: Francisco Seco/Reuters

Viongozi mbalimbali wameendelea kumtakia heri rais Trump na miongoni mwao ni kansela wa Ujerumani Angela Merkel kupitia msemaji wake aliemtakia uponyaji wa haraka rais Trump na mkewe. Pamoja naye ni waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson aliyeandika kwenye ukurasa wa Twitter akimtakia Trump na mkewe Melania uponyaji wa haraka.

Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence pia ameandika kwenye Twitter akisema wanawaombea wapone haraka akiungana na mamilioni ya Wamarekani kuwaombea.

Kutoka Geneva, Uswisi mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Tedros Adhanom Gebreyesus pia aliandika kupitia Twitter akimtakia kila lenye heri rais Trump na mkewe pamoja na uponyaji wa haraka. Trump mara kwa mara alilishutumu shirika hilo kwa kushindwa kukabiliana vyema na kusambaa kwa COVID-19 na kueleza nia yake ya kuliondolea ufadhili huku ikidai shirika hilo linaipendelea China.

Soma Zaidi: Rais Donald Trump alilaumu Shirika la Afya Duniani WHO

Ikulu ya Kremlin ya Urusi kupitia msemaji wake Dmitry Peskov pia imemtakia uponyaji wa haraka rais Trump, na kuongeza kuwa rais Vladmir Putin anatarajia kupata chanjo dhidi ya maradhi hayo lakini itatangaza atakapopata chanjo hiyo.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kama ilivyo kwa mamilioni ya Waisrael, yeye na mkewe Sarah pia wanawatakia afueni ya haraka marafiki zao huku Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel ambaye pia aliwatakia uponyaji wa haraka akisema hivi ni vita ambavyo wote wanaendelea kupigana navyo kila siku.

Mashirika: AFPE/APE/RTRE