1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Jumuiya ya ECOWAS kuujadili mgogoro wa Mali

Zainab Aziz Mhariri: Sudi Mnette
29 Mei 2021

Viongozi na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), wanakutana Jumapili nchini Ghana kujadili mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Mali.

https://p.dw.com/p/3u9rg
Ghana ECOWAS | Flaggen
Picha: AFP/N. Dennis

Rais Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane walijiuzulu nyadhfa zao baada ya kuwekwa kiuzizini kwa siku kadhaa juma hili, katika mapinduzi ambayo yanatajwa kupangwa na Goita, ambaye alijitangaza kuwa rais mara moja. Viongozi hao wa serikali ya mpito ya Mali rais Bah Ndaw na waziri mkuu Moctar Ouane walaichiwa baada ya kukaa kizuizini kwa muda wa siku tatu.

Wakati huo huo jamii ya kimataifa inaendelea kulishinikiza jeshi kurudisha utawala wa serikali ya mpito inayoongozwa na raia kuelekea uchaguzi utakaozingatia demokrasia baada ya mapinduzi ya mwaka jana.

Kanali Assimi Goita aliyejitangazwa na Mahakama ya Katiba kuwa Rais wa Mali
Kanali Assimi Goita aliyejitangazwa na Mahakama ya Katiba kuwa Rais wa MaliPicha: AP Photo/picture alliance

Jumuiya hiyo ya ECOWAS imeonya juu ya kuweka tena vikwazo dhidi ya mwanachama mwenza Mali baada ya wanajeshi mapema wiki hii kuwashikilia viongozi wa serikali ya mpito iliyopewa jukumu la kuurudi utawala wa kiraia baada ya mapinduzi hayo ya Agosti mwaka uliopita.

Mahakama ya Katiba ya Mali imemtangaza Kanali Assimi Goita, ambaye aliongoza mapinduzi ya kijeshi kuwa rais wa mpito. Katika uamuzi wake mahakama hiyo imesema Goita anapaswa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Rais Bah Ndaw ambaye amejiuzulu.

Rais wa Mali aliyejiuzulu Bah N'Daw, aliwahi kuwa waziri wa ulinzi kutoka mwaka 2014 hadi mwaka 2015 na pia alishikilia nafasi zingine kadhaa za kijeshi.

Rais wa mpito wa Mali aliyejiuzulu Bah Ndaw
Rais wa mpito wa Mali aliyejiuzulu Bah NdawPicha: Amadou Keita/Reuters

Uamuzi huo unazidisha mkwamo ambapo viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wanasema, unahatarisha harakati za kuelekea kwenye demokrasia na unadhoofisha mapambano dhidi ya makundi ya waasi.

Jumuiya ya ECOWAS yenye mataifa 15 imekuwa ikisimama na kutoa matamko imara katika mizozo kadhaa ya hivi karibuni katika eneo la Afrika Magharibi, iliweka vikwazo dhidi ya Mali baada ya maafisa vijana kumlazimisha kuachia madaraka rais aliyechaguliwa wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keita, baada ya kufanyika maandamano makubwa ya kumpinga.

Jumuiya hiyo iliisimamisha Mali kutoka kwenye vyombo vyake vya maamuzi, ilifunga mipaka yake na nchi hiyo na kusimamisha shughuli za fedha na biashara isipokuwa kwa bidhaa muhimu tu kama mafuta ya petroli na umeme.

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Mali aliyejiuzulu Moctar Ouane
Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Mali aliyejiuzulu Moctar OuanePicha: Raveendran/AFP/Getty Images

vikwazo hivyo viliondolewa baada ya serikali ya mpito kuundwa na kuwepo rais na waziri mkuu wa kiraia, na jeshi liliahidi kuurejesha utawala kamili wa raia ndani ya miezi 18.

Mali moja kati ya nchi masikini zaidi ulimwenguni, inapambana na waasi ambao walianza vurugu kwenye eneo la kaskazini mwa nchi hiyo mnamo mwaka 2012, baadaye uasi huo uliota mizizi na kuenea hadi katikati ya nchi hiyo na kisha kuvuka na kuingia katika nchi jirani za Niger na Burkina Faso. Maelfu ya watu wamekufa, na maelfu wengine wameyakimbia makazi yao.

Vyanzo:Afp/dpa