1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Korea Kaskazini na kusini wamaliza mkutano

Saumu Mwasimba3 Oktoba 2007

Viongozi wa Korea kaskazini na Kusini watarajiwa kutoa taarifa ya mwisho kesho alhamisi huku Korea kaskazini ikitangaza kuharibu kinu chake cha Kinuklia cha Yongbyong

https://p.dw.com/p/CH7C
Picha: AP

Viongozi wa Korea kusini na Kaskazini wamemaliza mkutano wao na wanajiandaa kutoa taarifa ya mwisho hapo kesho juu ya makubaliano yao katika mkutano wa kilele wa siku ya tatu kati yao.

Taarifa hizi zimekuja wakati ambapo Korea kaskazini imekubali kuharibu kinu chake kikuu cha kinuklia pamoja na kufafanua zaidi juu ya mpango wake wa kinuklia ifikapo tarehe 31 Desemba.

Mkutano kati ya viongozi wa Korea zote mbili Kusini na kaskazini ambazo bado kimsingi zipo katika vita ni wapili kuwahi kufanyika.Viongozi hao walitarajiwa kujadili mizozo ya mipaka ya baharini na ushirikiano wa kiuchumi.Awali rais Roh Moo-Hyun wa korea kusini alisema anataraji mkutano huu wa kilele utamaliza mivutano kati ya nchi hizo mbili lakini mambo yanaonyesha kama matarajio ni machache mno.

Rais wa Korea kaskazini Kim Jong iLL alipendekeza kwamba mwenzake wa Korea Kusini Roh Moo-Hyun aendelee kubakia kaskazini kwa siku moja zaidi kwa ajili ya mazungumzo lakini vyombo vya habari vya Korea Kusini vimesema kwamba bwana Roh amekataa ombi hilo.

Taarifa zinasema baada ya kumalizika mazungumzo ya leo Kim Jong Ill alisema majadiliano yamekuwa marefu na kwamba taarifa ya mwisho itatolewa kama ilivyopangwa.

Hata hivyo hakuna maelezo yaliyotolewa juu ya mada zilizojadiliwa lakini inafikiriwa mazungumzo hayo yaligusia zaidi juu ya kuweka mipaka ya baharini suala ambalo limesalia kuleta mivutano tangu mzozo wa mwaka 1950 hadi 1953.

Wakati wa mapumziko ya kikao cha leo rais Roh Moo Hyun wa korea kusini alisema mazungumzo ya asubuhi yalikuwa ya wazi nay a kweli lakini akaongeza kwamba pande zote mbili inabidi zijifunze kuaminiana.

Aidha alisema serikali ya mjini Pyongyang imeeleza kutoridhishwa kwake na kasi ya kuundwa eneo la kiviwanda la pamoja shughuli inayoendeshwa na Korea Kusini huko Kaesong.

Wakati hayo yakiarifiwa maafisa wa China wamesema Korea kaskazini imekubali kuharibu kinu chake kikubwa cha Kinuklia pamoja na kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu shughuli zake zote za kinuklia ifiakiapo tarehe 31 Desemba.

Tangazo la Korea kaskazini limekuja baada ya mazungumzo ya pande sita yaliyofanyika wiki iliyopita mjini Beijing China.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Wu Dawei ambaye aliongoza mazungumzo hayo ya pande sita amesema Marekani itahusika kuongoza shughuli za kuharibu kinu hicho cha Kinuklia cha Yongbyon.

Mwaka uliopita Korea kaskazini ilifanya majaribio ya kombora la Kinuklia lakini ilikubali kukomesha mpango wake wa Kinuklia kwa sharti itapewa msaada wa kiuchumi na faida nyingine za kidiplomasia.

Rais Bush wa Marekani ni wa mwanzo kuipongeza hatua ya Korea kaskazini akisema nchi hiyo iliyotengwa sasa itapokea kiasi cha tani millioni moja ya mafuta ghafi na pia itaondolewa katika orodha ya Marekani ya nchi zinazounga mkono Ugaidi.Japan pia imeipongeza hatua iliyochukuliwa na Korea kaskazini ikisema sasa nchi hiyo itathaminiwa.

Marekani imesema itawatuma katika kipindi cha wiki mbili zijazo wataalamu wake Korea Kaskazini kwa ajili ya kuanza matayarisho ya kuharibu kinu hicho cha Yongbyong.Korea Kaskazini kwa upande mwingine imesisitiza kwamba haitahamisha bidhaa zozote za kinuklia,technologia wala ufundi kwa nchi nyingine lakini pia imetaka kujua lini itaondolewa kutoka orodha ya Marekani ya nchi za Kigaidi.